Watanzania waadhimisha Uhuru kwa shughuli za kijamii

TANZANIA leo inaadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania bara.

Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza maadhimisho hayo yafanyike katika ngazi ya mikoa na fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili ya maadhimisho hayo zitumike kutoa huduma za kijamii.

Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara yanafanyika yakibeba kaulimbiu, “Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi wa maendeleo yetu”.

Advertisement

Sherehe za Uhuru mwaka huu zilianza Desemba 2, mwaka huu hazitakuwa na gwaride na shughuli nyingine za kitaifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza kila mkoa uhakikishe wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ukiwamo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii yakiwamo masoko, hospitali, kambi za wazee na wenye mahitaji maalumu.

Alitaja shughuli nyingine ni mashindano ya michezo na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu ambayo nchi imefikia katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru.

“Ninatoa rai kwa wakuu wote wa mikoa ya Tanzania Bara kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo mahususi yaliyotolewa na serikali ili kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo la kuuenzi Uhuru wetu,” alisema Majaliwa Dodoma.

Aliongeza: “Taasisi zote za serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama zinaelekezwa kuhakikisha majengo yote ya serikali Tanzania Bara yanapambwa kwa vitambaa vya rangi ya Bendera ya Taifa, picha rasmi ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere ambaye ni muasisi wa Uhuru wetu pamoja na picha ya Rais Samia Suluhu Hassan.”

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika, Nyerere alisema alihimiza watu wafanye kazi ili kumaliza umasikini.

“Mara nyingi sana nimesema nanyi juu ya umasikini, ujinga na maradhi, lakini kwa kweli adui yetu mkubwa ni umasikini,” alisema Nyerere.

Aliongeza: “Tukiweza kumshinda adui huyu, tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi. Lakini ni ninyi tu, tunaoweza kupigana vita vya umasikini. Namuomba kila raia wa Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umasikini”.

Aliongeza: “Bila umoja hatuna nguvu ya kuendelea na jambo lolote… wala tusipoteze wakati wetu katika kugombania vyeo na fahari ya nafsi. Kilichotufikisha hapa leo kwa upesi hivi na kwa amani hivi ni umoja wa watu wa Tanganyika”.