Watanzania waaswa kujilinda dhidi ya utapeli wa fedha kwa simu

DAR ES SALAAM: WATANZANIA wametakiwa kuongeza umakini katika matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu ili kujilinda dhidi ya utapeli na wizi wa taarifa binafsi, wakati matumizi ya huduma hizo yakiendelea kuongezeka nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi Juni 2026 kulikuwa na akaunti milioni 87 za huduma za fedha kwa njia ya simu nchini, huku majaribio 7,334 ya udanganyifu yakirekodiwa katika kipindi hicho.

Ingawa idadi hiyo ilipungua kwa asilimia 25.29 ikilinganishwa na robo iliyotangulia, kampuni za mawasiliano zimeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua tahadhari katika kulinda akaunti zao na taarifa binafsi.

Vodacom Tanzania PLC imesema usalama wa mteja unaanzia katika kuhakikisha kuwa mtu sahihi ndiye anayepata huduma kwenye akaunti husika, ikiwa ni pamoja na uthibitishaji wa utambulisho wakati wa usajili na mabadiliko ya laini za simu.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa usajili wa laini unahusisha uthibitishaji wa alama za vidole dhidi ya taarifa za NIDA, huku mabadiliko ya laini yakifanyika na mhusika mwenyewe, hatua inayolenga kuzuia watu wasiohusika kuchukua udhibiti wa akaunti za wateja.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Shughuli za Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania PLC, Harriet Lwakatare, alisema kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kidijitali kunaenda sambamba na wajibu wa kuhakikisha fedha na taarifa za wateja zinalindwa.

“Wateja wetu wanatuamini na kutukabidhi sehemu muhimu za maisha yao ya kila siku, ikiwemo fedha zao na taarifa zao binafsi. Imani hiyo inakuja na wajibu wa kuhakikisha wateja wetu wako salama,” alisema Lwakatare.

Alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja, inayofanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, inatoa nafasi kwa kampuni kuwaelimisha wateja kuhusu hatua za usalama, pamoja na kuwahimiza kushiriki katika kulinda akaunti zao.

Vodacom imewakumbusha wateja kutompa mtu yoyote namba za siri za huduma za fedha, hata kama mtu huyo anajitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa kampuni hiyo.

Aidha, imewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini au kuhisi wamekumbana na tukio la udanganyifu, ili hatua za ufuatiliaji ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, timu yake inayoshughulikia masuala ya udanganyifu hushirikiana na wateja kufuatilia namba za simu au barua pepe zinazohusishwa na matukio yanayoripotiwa na, pale inapohitajika, hushirikiana na Jeshi la Polisi katika uchunguzi.

Vodacom imesisitiza kuwa teknolojia za usalama pekee hazitoshi bila uelewa wa mtumiaji, hivyo wananchi wanapaswa kutunza siri za taarifa zao, kutotoa namba za siri na kuripoti haraka shughuli wanazoziona kuwa si za kawaida katika akaunti zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button