Watanzania wanaamua

WANANCHI wa Tanzania leo wanapiga kura kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano.

Hivi karibuni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka alitoa taarifa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha leo iwe siku ya mapumziko kuwawezesha wananchi wenye sifa stahiki kupiga kura.

Balozi Kusiluka alieleza uamuzi huo ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Rais chini ya Sheria ya Sikukuu za Kitaifa Sura ya 35.

Uchaguzi wa leo ni wa kwanza tangu kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliyochukua majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Vyama vinavyoshiriki

Vyama 18 vyenye usajili wa kudumu vinashiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu vikiwemo 17 vyenye wagombea wa nafasi ya urais.

Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) hakina mgombea wa nafasi ya urais ila kina wagombea kwenye nafasi za ubunge na udiwani.

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakishiriki uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa hakikusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.

Vyama vingine vinavyoshiriki ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Chama cha Demokrasia Makini (MAKINI), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Democratic Party (DP).

Vingine ni Alliance for African Farmers Party (AAFP), United Democratic Party (UDP), Union for Multiparty Democracy (UMD), Tanzania Democratic Alliance (ADA-TADEA), United People’s Democratic Party (UPDP) na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huu ni National League for Democracy (NLD), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for Democratic Change (ADC), National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Chama cha Kijamii (CCK) na Tanzania Labour Party (TLP).

Uchaguzi wa saba

Julai 26 mwaka huu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza ratiba ya uchaguzi huo wa saba tangu kurudishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania mwaka 1992.

INEC ilitangaza ratiba hiyo kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 41 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 41 (1) na 49 (1) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na 1 ya Mwaka 2024,

Uchaguzi Mkuu wa kwanza ulifanyika mwaka 1995, ukafuata wa 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020.

Katika chaguzi zote hizo kwenye nafasi ya urais walishinda wagombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 1995 na 2000 alishinda Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, mwaka 2005 na 2010 alishinda Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na mwaka 2015 na 2020 alishinda Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kulikuwa na wagombea 15 wa urais akiwemo Magufuli kupitia CCM aliyepata kura 12,516,252, Tundu Lissu kupitia Chadema aliyepata kura 1,933,271, Lucas Mahona kupitia NRA kura 80,787, John Shibuda kupitia ADA-Tadea kura 33,086, Muttamwega Mgaywa kupitia SAU 14,922 na Queen Sendiga kupitia ADC kura 7,627.

Wengine ni Cecilia Mmanga kupitia MAKINI kura 14,556, Yememia Maganja kupitia NCCR-Mageuzi kura 19,969, Ibrahim Lipumba kupitia CUF kura 72,885, Philipo Fumbo kupitia DP kura 8,283, Bernard Membe kupitia ACT Wazalendo kura 81,129, Twalib Kadege kupitia UPDP kura 6,194, Hashim Rungwe kupitia Chaumma kura 32,878, Seif Seif kupitia AAFP kura 4,635 na Mohamed Mazrui kupitia UMD kura 3,721

Idadi ya wapigakura, vituo, majimbo

INEC imetangaza wapigakura 37,647,235 wameandikishwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Ramadhani Kailima alisema idadi hiyo ya wapigakura 37,647,235 ni sawa na ongezeko la asilimia 26.53 kutoka idadi ya wapigakura 29,754,699 waliokuwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2020.

Kailima alieleza kuwa kati ya wapigakura 37,647,235, wapigakura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapigakura 996,303 wapo Zanzibar.

Alisema kati ya wapigakura 37,647,235 wanawake ni 18,950,801 sawa na asilimia 50.34 na wanaume ni 18,696,439 sawa na asilimia 49.66.

Kailima alisema Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) limeandikisha wapigakura 717,557.

Alisema katika uchaguzi wa leo vituo vya kupigia kura vitakavyotumika ni 99,895 sawa na ongezeko la asilimia 22.47 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kailima alisema vituo 97,348 vipo Tanzania Bara na 2,547 vipo Zanzibar.

Awali Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele alisema majimbo yatakayotumika kwenye uchaguzi ni 272 yakiwemo 222 ya Tanzania Bara na majimbo 50 yapo Zanzibar huku kukiwa na ongezeko la majimbo manane yaliyoanzishwa Tanzania Bara.

 Kanuni za maadili

Katika mchakato wa uchaguzi huo vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) walisaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025.

Kanuni hizo zilitengenezwa kwa kuzingatia Kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na 1 ya mwaka 2024.

Kanuni hizo zimeweka msingi wa kuzingatiwa na washiriki wa uchaguzi na hatua za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa kwa atakayekiuka vikiwemo vyama vya siasa, wagombea, INEC na serikali.

 Wafungwa, mahabusu kupiga kura

INEC imesema kwa mara ya kwanza wafungwa na mahabusu watapiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Kailima alisema wafungwa na mahabusu watapiga kura ya urais pekee na katika maeneo hayo hakutakuwa na mawakala wa vyama vya siasa.

 Maelekezo ya INEC

Hivi karibuni ilitangazwa kuwa mpigakura asiye na picha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini ana kadi ya mpigakura yenye taarifa zinazofanana na zilizomo kwenye daftari hilo ataruhusiwa kupiga kura.

Pia, ilielezwa mpigakura mwenye kadi yenye namba tofauti na iliyopo kwenye daftari hilo lakini taarifa nyingine zote zikiwa sawa ikiwemo jina na picha ataruhusiwa kupiga kura.

Kailima alieleza mpigakura ambaye ameandikishwa na taarifa zake zipo kwenye daftari husika lakini amepoteza au kuharibu kadi yake, ataruhusiwa kupiga kura kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa (NIDA), leseni ya udereva au pasi ya kusafiria ili mradi majina yaliyopo kwenye kitambulisho yanafanana na yale yaliyo katika daftari.

Aliagiza mpigakura mwenye kadi ya kupigia kura lakini taarifa zake hazipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura asiruhisiwe kupiga kura.

 Waangalizi wa uchaguzi

INEC imetoa vibali vya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu kwa taasisi na asasi 76 za kiraia za ndani na 12 za kimataifa.

Jaji Mwambegele alisema pia INEC ilitoa kibali cha kutoa elimu ya mpigakura kwa taasisi na asasi za kiraia 164 za ndani.

Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari aliwataka waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wazingatie sheria za nchi na waepuke kuingilia au kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuathiri au kuingilia mchakato wa uchaguzi.

Jaji Asina alisema waangalizi hao wanapaswa kutekeleza majukumu kwa uadilifu, uhuru, wasiwe na upendeleo na wazingatie sheria za nchi na Mwongozo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa mwaka 2025.

“Waangalizi wanapaswa kuepuka kuingilia shughuli za uchaguzi, kutoonyesha dhihaka kwa watendaji wa uchaguzi, au kutoa maelekezo kwa maafisa wa Tume kuhusu namna ya kufanya kazi zao,” alisema.

Amani, Usalama

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema kutakuwa na amani, usalama na utulivu wakati wa mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Benard Mlunga alieleza JWTZ inawahakikishia Watanzania hali ya amani, usalama na utulivu kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

 TCRA yaagiza sms zilinde amani

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa mwongozo kuhusu usambazaji wa maudhui na arafa (ujumbe mfupi kwa simu za mkononi) za mkupuo kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari aliagiza wadau wote wahakikishe maudhui wanayopeleka kwa wananchi yanadumisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.

Dk Bakari alikumbusha watoa huduma za mawasiliano ya simu na wanaoandaa arafa wahakikishe maudhui ya arafa za mkupuo kuelekea, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 yanazingatia sheria na kanuni zote za mawasiliano ya kielektroniki na posta.

Aliagiza maudhui yote yanayohusiana na shughuli za Uchaguzi Mkuu yapate idhini kutoka kwa taasisi au uongozi wa chama cha siasa husika.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 6000-12700 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..

    .

    This is my main concern……………………………………. http://Www.Cash43.Com

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us →→→→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button