Watoto 29 wazaliwa mkesha wa Pasaka

DAR ES SALAAM; WATOTO 29 wamezaliwa katika Hospitali ya Taifa Upanga, Mloganzila, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Temeke na Amana katika usiku wa mkesha wa Pasaka.
Ofisa habari wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, Florian Godwin alilieleza HabariLEO jana kuwa katika hospitali hiyo watoto 10 walizaliwa kuanzia usiku wa mkesha wa Pasaka hadi asubuhi, wa kiume walikuwa watano na wa kike watano.
Alisema kati ya watoto hao 10, saba walizaliwa kwa njia ya kawaida, wa kike watatu na wa kiume wanne na watatu walizaliwa kwa njia ya upasuaji huku wa kike wakiwa wawili na wa kiume mmoja.
Alisema watoto wote waliozaliwa katika usiku huo wanaendelea vizuri, wao pamoja na wazazi wao.
Kwa upande wa Hospitali ya Mkoa Mwananyamala, Ofisa habari wa hospitali hiyo, Onesmo Milanzi alieleza kuwa watoto sita walizaliwa, wa kike wakiwa wanne na wa kiume wawili.
Milanzi alisema katika watoto hao sita, watano walizaliwa kwa njia ya kawaida na mmoja alizaliwa kwa njia ya upasuaji huku afya zao zikiwa zinaendelea vizuri.
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, watoto waliozaliwa katika usiku wa Pasaka ni wawili wote wa kiume na walizaliwa kwa njia ya upasuaji.
Kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, walizaliwa watoto 10 wa kike wanne na wa kiume sita.
Kwa mujibu wa msimamizi wa zamu wa hospitali hiyo, Ismail Hamis alilieleza HabariLEO kuwa kati ya watoto hao 10, sita walizaliwa kwa njia ya kawaida na wanne walizaliwa kwa njia ya upasuaji.
Kwa ujumla watoto wote waliozaliwa katika mkesha wa Pasaka wapo katika afya njema na wanaendelea vizuri.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Upanga, Angela Mndolwa alisema katika mkesha huyo amezaliwa mtoto mmoja wa kiume.



