Watoto 600 wafanyiwa upasuaji wa kichwa kikubwa

DAR ES SALAAM: Jumla ya watoto 4,000 wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi wametibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku 600 kati yao wakifanyiwa upasuaji.
Mkurugenzi Msaidizi wa Upasuaji wa hospitali hiyo, Dk Godlove Mfuko, amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi, yaliyoandaliwa na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi Tanzania (ASBAHT) katika hospitali hiyo.
Dk Mfuko amesema hospitali hiyo imeendelea kuimarisha huduma za matibabu na upasuaji kwa watoto wenye changamoto hizo kwa kuongeza idadi ya wataalamu bingwa, wakiwemo waliobobea katika upasuaji wa mfumo wa fahamu kwa watoto kupitia Mpango wa Samia wa Mafunzo ya Ubingwa wa Juu katika sekta ya afya.

Amesema hospitali hiyo inalenga kuwa kituo cha umahiri katika upasuaji wa mfumo wa fahamu kwa watoto, sambamba na kutenga chumba maalumu kwa ajili ya upasuaji wa watoto kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma hizo.
Aidha, amesema hospitali inalenga kuhakikisha watoto wanaohitaji upasuaji wanapata huduma ndani ya saa 48 baada ya kufika hospitalini, kulingana na tathmini ya hali zao za kiafya na mahitaji ya matibabu.
Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza umuhimu wa wanawake wanaopanga kupata ujauzito na wajawazito kutumia madini ya foliki (folic acid) kwa ushauri wa wataalamu wa afya ili kupunguza hatari ya watoto kuzaliwa na kasoro za ukuaji wa mfumo wa fahamu, ikiwemo mgongo wazi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mwinyi Kondo Juma, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Tiba amewahimiza wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kinga, utambuzi na matibabu ya changamoto hizo ili watoto wapate huduma kwa wakati.
Amesema elimu sahihi itasaidia kuondoa imani potofu zinazohusisha hali ya kichwa kikubwa na mgongo wazi na uchawi au laana, huku akihimiza jamii kuwapa watoto hao upendo, matunzo na msaada unaohitajika badala ya kuwabagua na kuwanyanyapaa.

Dk Juma amesisitiza kuwa ulemavu haupaswi kuwa kikwazo cha kupata haki na fursa, akihimiza watoto na watu wenye ulemavu kupata fursa sawa katika huduma za afya, elimu na shughuli nyingine za kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi, familia zao kutoka mikoa mbalimbali, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu kinga, matibabu, malezi na ustawi wa watoto hao, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kuboresha huduma zao.



