Watoto 67% wanatumia mitandao ya kijamii

ASILIMIA 67 ya watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 17 wanatumia mitandao ya kijamii na asilimia nne kati yao wakikabiliwa na ukatili wa aina mbalimbali.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Sebastian Kitiku alisema hayo wakati akitoa mada kuhusu malezi na makuzi ya watoto na vijana uliofanyika kwenye mtandao wa X.
Alisema licha ya kuwepo kwa miongozo mbalimbali, bado kuna changamoto katika malezi na makuzi ya watoto na vijana na kwamba wazazi na walezi wanapaswa kusimamia wajibu wao.
Alisema matokeo hayo ni ya utafiti walioufanya mwaka 2022 wakishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Alisema asilimia kubwa ya watoto wanapopata simu wanaangalia maudhui yanayohusiana na ngono hivyo kuamsha hisia za kufanya ngono katika umri mdogo na matokeo yake hupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na magonjwa zinaa.
Pia, alisema watoto wanapoachiwa simu hujiingiza katika mila na desturi zisizofaa na kuchangia mmomonyoko wa maadili unaoenda sambamba na mitindo ya maisha isiyofaa.
“Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto husababisha wanaingia kwenye usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, ugaidi, panya road hivyo bila uangalizi wataingia kwenye makundi hayo,” alisema.
Kitiku alisema watoto wanarubuniwa kwa kuwasiliana na wahalifu ambao huwataka kukutana au kuwataka kurekodi picha za ngono na kuwapatia ujira mdogo.
“Picha wanazotuma hubadilika na kuwa silaha ya kuadhibiwa kwa vitisho kwamba zitasambazwa mitandaoni hivyo hupata taharuki endapo wazazi wao na jamii inayowazunguka ikiziona. Hufanya maamuzi ya kujiua, wengine hupata msongo wa mawazo,” alisisitiza.

Kadhalika alisema matumizi ya simu huwafanya watoto kuwa waraibu wa mitandao na kusahau kazi za nyumbani na kusahau masomo yao.
Alishauri wazazi na walezi wasiruhusu kuwaachia watoto simu bila uangalizi wa karibu na badala yake wawaongoze kuhusu matumizi sahihi ya simu.
Pia, aliwataka kutoruhusu watoto wawaongoze katika matumizi ya simu kwamba madhara ya matumizi ya simu hutokana na kuwaachia kulala nazo vyumbani kwani huchangia kushindwa kulala na kuangalia maudhui yasiyofaa.
Kitiku alieleza kwamba sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008, inaelekeza mtoto alelewe na akue kwa kuhakikisha haki yake ya kuishi, kuendelezwa kielimu na haki ya kulindwa asifanyiwe ukatili.
Aliongeza kuwa watoto wa umri chini ya miaka nane na rika la vijana balehe linaloanzia miaka tisa hadi 18 linahitaji uwekezaji mkubwa kuwa na watoto wenye uwezo mkubwa wa kufikiria na kupambanua mambo.



