Watoto wa Sarungi, viongozi watoa ya moyoni

WATOTO wa kiongozi mstaafu serikalini, Profesa Philemon Sarungi wamesema baba yao alikuwa mwalimu kwao.
Watoto hao, Martin, Emock, Veronica na Maria wamesema baba yao hakuwa tajiri wa mali bali wa watu.
Walisema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa baba yao katika viwanja vya Karimjee kabla ya maziko kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Martin, Emock na Maria hawakuhudhuria maziko ya baba yao kwa kuwa wapo nje ya nchi hivyo walituma salama zao kwa ujumbe wa sauti kutoa salamu zao za mwisho kwa kiongozi huyo.
Maria kupitia sauti, alisema baba yao aliwahi kuwaeleza kuwa maisha ni mapambano na bila kufanya hivyo hawataweza kufikia mafanikio yao.
“Ingawa sitaweza kuja kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu za kiusalama, nina imani kuwa ipo siku tutaonana ahera baba,” alisema.
Maria alisema baba yao alikuwa mwalimu wa maisha yao na wameshuhudia akiendelea kukutana na watu hata baada ya kustaafu na hakuacha kumsaidia yeyote aliyemuomba msaada.
“Hakuwahi kuwa tajiri wa mali, lakini alikuwa tajiri wa watu na mahusiano na uwepo wenu hapo ni ushuhuda wa utajiri wake wa upendo na heshima aliyojijengea katika jamii,” alisema.
Maria alisema baba yao amewajengea uaminifu, imani na hofu ya Mungu na zaidi aliipenda Tanzania na kuwajenga katika msingi wa kuitumikia nchi na si kujinufaisha.
Mtoto wa kwanza wa Profesa Sarungi, Dk Emock ameshukuru kwa maisha ya baba yake akisema anaamini ataendelea kuwa katika maisha yao hasa kwa kuwa kuna wajukuu wake.
“Nakupenda na nitakukumbuka, tunakupenda na tutakukumbuka, Mungu akuweke mahala pema peponi,” alisema Emock.
Martin alisema atamkumbuka baba yake kwa malezi bora na ataendelea kuenzi mafunzo aliyompatia.



