Watu 19 mbaroni kwa kuwarubuni vijana kuwa mabilionea

POLISI mkoani Morogoro imekamata watu 19 kutoka kwenye kampuni nne zilizopo mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuwarubuni mamia ya vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini kupitia mitandao ya kwamba wanawafundisha namna ya kuwa mabilionea.

Vijana hao wanapofika kwenye kampuni hizo hutakiwa kulipa ada ya Sh 600,000 hadi Sh milioni moja na kisha huwaweka kambini kwa madai ya kuendelea na masomo zaidi na wakiaminishwa watakapohitimu watapata ajira kupitia mtandao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alisema hayo jana kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu baada ya kufanyika operesheni za kukabiliana na matapeli sugu ambao wanatumia mtandao kuwarubuni vijana kupitia mitandao.

Alisema vijana 399 wameshaokolewa kutoka mikononi mwa matapeli hao ambapo tayari watuhumiwa zaidi ya 19 wanaohusika na utapeli huo wamekamatwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, vijana wengi wanatokea mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Mwanza na Iringa.

Mkama alitaja kampuni zinazotumika kuwarubuni vijana hao ambazo zinachunguzwa kuhusu uhalali wake ni Kampuni ya Alliance in Motion Global, QY Group of Company, Q-Net Group of Companies na Kampuni ya Instant Milionea.

“Kwa sasa viongozi wa kampuni hizo wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema na kuongeza kampuni hizo zinawarubuni vijana hao kwa kuwashawishi kufika eneo watakakoelekezwa ili wapate mafunzo ya ujasiriamali ama wawe mabilionea ambapo hulipa ada kati ya Sh 600,000 hadi milioni moja.

Alisema kuwa wakishapokelewa hupelekwa kwenye kambi ambazo ni nyumba kubwa yenye uzio na si rahisi kuonekana na watu wengine.

Kamanda Mkama alieleza zaidi kuwa watu hao kisha huanza kuwalazimisha wakashawishi wenzao ambao huwatafuta na kuwapa maneno mazuri na kusafiri kufika kambini Mkoa wa Morogoro.

Aliwataka wazazi wasiwaruhusu vijana wao kwenda mkoani Morogoro kufanya mafunzo ambayo hayatambuliki na taratibu za serikali na hakuna mafunzo ya kumfanya mtu kuwa bilionea kwa utaratibu unaofanywa na hao matapeli.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button