Watu 47 wanaswa vitendo vya kihalifu

JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limewakamata watu 47 kwa kipindi cha mwezi Oktoba 2024 kwa tuhuma mbalimbali za kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam Jumanne Muliro amesema Oktoba 29/2024 walikamatwa watuhumiwa kumi na tano (15) kwa tuhuma za wizi wa kontena lililokuwa na vifaa vya kuchimbia madini mali ya Kampuni ya MKUTI LTD ambavyo vilikuwa vinasafirishwa kutoka Dar es salaam kwenda Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.

Amevitaja vifaa hivyo kuwa ni engine machine 07, Digger machine 15, vibuyu vya compresser 90, na Atometer machine 02.

Advertisement

Kamanda Muliro amesema Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kisheria baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa siku za nyuma na baadae kufikishwa mahakamani wamepatikana na hatia akiwemo Derick Kiyagoka (32) Mkazi wa Kitunda Kati aliyehukumiwa miaka 30 jela na Mahakama ya Kinyerezi kwa kosa la kubaka.

Wengine ni Saidi Kambi (49) mkazi wa Mbagala alifikishwa kwenye Mahakama ya Kinyerezi na kuhukumiwa kifungo cha Maisha jela kwa kosa la Kubaka na Kulawiti, Saidi Abdallah alihukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti baada ya kufikishwa kwenye mahakama ya Wilaya Kinondoni, Ayubu Saidi pia alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa Unyanganyi wa kutumia silaha kwenye mahakama ya Wilaya Kinondoni.

Pia Abdala Athumani miaka 31 mkazi Yombo alisomewa hukumu ya kunyongwa hadi kufa na mahakama ya wilaya ya Kigamboni kwa kosa la mauaji, Iddy Omary Ndekae miaka 26 mkazi wa Mbagala alihukumiwa hukumu ya kunyongwa hadi kufa na mahakama ya wilaya ya kigamboni kwa kosa la mauaji.

Aidha ameongeza kuwa Jumla ya watuhumiwa 22 walikamatwa kwa kujihusisha na kusafirisha, kuuza na kutumia dawa za kulevya ikiwemo bangi.

Pia wamekamatwa watu 10 kwa tuhuma za kujihusisha na uvunjaji wa nyumba mchana na usiku baadae kuiba.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi lao ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ili kuziba mianya ambayo wahalifu wanaweza kutumia kutenda uhalifu.