Watu 7,000 wafa DR Congo

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Judith Tuluka ametangaza zaidi ya watu 7,000 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa mwaka huu kutokana na mapigano.
Amesema mapigano hayo ni kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Waasi hao, wakiongozwa na kundi la M23, waliteka miji miwili mikubwa katika maeneo hayo, na kuacha athari kubwa kwa raia.
Wiki iliyopita, wapiganaji wa M23 walichukua udhibiti wa Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini. Hali hiyo ilifuatia kushindwa kwa jeshi la DRC kulinda mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Gom ambao ulitekwa mwishoni mwa mwezi uliopita. Hali ya usalama imeendelea kuwa mbaya, na mapigano ya mara kwa mara yameleta hofu kubwa kwa raia.
Waziri Mkuu Judith Tuluka aliwaambia wajumbe wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu mjini Geneva kwamba hali ya usalama mashariki mwa DRC imefikia kiwango cha kutisha.
Hali hii ya mivutano ya kijeshi mashariki mwa DRC imeendelea kuwa changamoto kubwa kwa serikali ya nchi hiyo, huku wakishindwa kudhibiti maeneo mengi yanayotawaliwa na waasi. Serikali ya DRC inaomba msaada wa kimataifa katika juhudi za kurejesha amani na usalama katika maeneo yaliyokumbwa na machafuko.



