Watuhumiwa 211 wakamatwa Kilimanjaro

KILIMANJARO: JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu 211 kwa tuhuma mbalimbali za uhalifu, ikiwemo wizi, kupatikana na dawa za kulevya, mirungi, uuzaji wa pombe haramu, kupatikana na nyara za serikali, pamoja na kuwakamata wahamiaji haramu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo, watuhumiwa hao walikamatwa katika misako na operesheni zilizofanyika kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Aidha jeshi hilo limeeleza kuwa kati ya kesi hizo, kesi 90 tayari zimefikishwa mahakamani, ambapo kesi 30 zimemalizika na watuhumiwa wamepewa adhabu mbalimbali kulingana na hatia zao.
Adhabu zilizotolewa kwa watuhumiwa hao ni pamoja na watuhumiwa wanne wamepewa adhabu ya kifungo cha maisha jela, huku wengine wanane wakihukumiwa kifungo cha miaka 30, watuhumiwa 40 wamehukumiwa vifungo vya kati ya miaka mitano hadi 2, huku watuhumiwa wawili wakihukumiwa kulipa faini.
Jeshi la Polisi limeongeza kuwa kesi 74 bado ziko katika hatua mbalimbali za usikilizwaji mahakamani.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limewasihi wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za wahalifu na vitendo vya uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wakati.



