Watuhumiwa 3 ujambazi wauawa kwa bunduki

KIGOMA; WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakituhumiwa kutaka kufanya tukio la ujambazi kwenye barabara kuu ya Kutoka Kasulu kuelekea Kibondo baada ya kufunga barabara kwa mawe makubwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu amesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku katika Kijiji cha Kigendeka Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, ambapo watuhumiwa hao wanadaiwa kutaka kufanya tukio la uhalifu la kuteka magari.

Kamanda Makungu amesema kuwa kabla ya kuuawa watuhumiwa hao kulitokea majibizano ya risasi baina ya majambazi hao na polisi, ambapo majambazi hao walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali ya wilaya Kibondo kwa matibabu na walifariki dunia baadaye.

Pamoja na kuuawa kwa majambazi hao Kamanda Makungu amesema kuwa eneo la tukio walikuta bunduki moja aina ya AK 47 ikiwa na magazine moja yenye risasi 10, bunduki moja iliyotengenezwa kienyeji, panga moja na marungu matatu.

Alisema kuwa majambazi hao waliweka mawe makubwa barabarani kwa nia ya kuteka magari ambayo yangepita kwenye barabara hiyo,  ambapo polisi walipata taarifa na kufika eneo la tukio kabla hayajatokea madhara na kufanikiwa kuzima tukio hilo la utekaji.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button