Watumia Bandari ya Mtwara kusafirisha makaa ya mawe
KAMPUNI ya wazawa ya Jitegemee Holdings Company Ltd, inayojihusha na uchimbaji wa madini nchini, imeanza kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha makaa ya mawe kwenda nje ya nchi.
Kampuni hiyo imeanza leo kwa kusafirisha tani 22,000 kwenda nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuanza shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa makaa hayo katika viwanda vya Tanzania, Kenya na Uganda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Emmanuela Kaganda, amesema Kampuni hiyo imeingia katika historia kubwa ya kusafirisha makaa ya mawe kwa kutumia bandari ya Mtwara, ambapo mwanzo walitumia usafiri wa barabara kupeleka kwenye viwanda vya ndani na nchi jirani za Kenya na Uganda.
‘’Safari hii tumepata bahati ya kuweza kusafirisha makaa ya mawe kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa kutumia bandari ya Mtwara,” amesema.
Kaganda amesema mwezi ujao meli nyingine ya tani 40,000, itasafirisha makaa mengine kupitia badari ya Mtwara kuelekea Falme za Kiarabu kwenye Kiwanda cha Saruji, ambapo pia Oktoba mwaka huu watasafirisha tani 50,000 kuelekea Ulaya.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas, ameipongeza kampuni hiyo ya Jitegemee kwa kuona fursa ya kutumia bandari ya Mtwara kusafirsha makaa hayo.
“Nimefarijika kuona kampuni ya kwanza ya Kizawa iliyothubutu kufanya uwekezaji huo mkubwa wa biashara ya makaa, ambayo yana soko kubwa duniani na sasa kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha,” amesema.
RC huyo ametoa wito kwa wasafirishaji wengine wa bidhaa nyingine ikwemo korosho, ambazo nyingi zinapatikana katika mikoa ya kusini na Mtwara kutumia bandari hiyo kwa sababu bandari hiyo kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali hasa upanuzi wa bandari uliogharimu bilioni 157.