Watumishi PCCB wanufaika mikopo bil 43/-

ARUSHA: PCCB SACCOS imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 43.2 kwa wanachama 5,522 katika kipindi cha mwaka mmoja, hatua inayolenga kuwawezesha watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujikwamua kiuchumi kupitia fursa za kifedha zinazotolewa na chama hicho.
Mikopo hiyo ilitolewa kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo elimu, ujenzi, biashara, uvuvi na mahitaji ya dharura.
Akizungumza leo jijini Arusha wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 23 wa PCCB SACCOS wa mwaka 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Cyprian Chalamila, amewataka viongozi wa chama hicho kusimamia kwa uadilifu na uaminifu fedha za wanachama ili kulinda maslahi yao na heshima ya taasisi.

Chalamila amesema mafanikio ya SACCOS hiyo ni jambo la kupongeza, akisisitiza kuwa viongozi wana wajibu wa kuhakikisha fedha za wanachama zinalindwa na kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto ya baadhi ya wanachama kuchelewesha marejesho ya mikopo, hali inayoweza kuathiri uwezo wa chama kutoa mikopo kwa wanachama wengine.
Amewataka viongozi kuchukua hatua stahiki kwa wanachama wanaoshindwa kurejesha mikopo kwa makusudi na kusisitiza kuwa watumishi wa TAKUKURU wanapaswa kuwa mfano wa kuzingatia maadili na kutimiza wajibu wao.

Aidha, amewahimiza watumishi 400 ambao bado hawajajiunga na PCCB SACCOS kujiunga ili wanufaike na fursa za mikopo na huduma nyingine za kifedha zinazotolewa na chama hicho.
Chalamila pia amesisitiza umuhimu wa wanachama kupata elimu ya bima, usimamizi wa fedha na uwekezaji ili kuongeza uelewa wao katika kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PCCB SACCOS, Betrod Busanda, amesema chama hicho kinatarajia kupata faida ya Sh bilioni 7.3 katika kipindi hicho, huku kikikusanya Sh milioni 565 za bima ya mikopo na Sh milioni 555 za kinga ya posho.

Busanda amesema wanachama 5,522 walipata mikopo hiyo kwa idadi ya mikopo iliyojumuisha wanachama waliokopa zaidi ya mara moja, huku wanachama 1,778 wakiwa wamekopa bila kujirudia.
Naye Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amewataka wanachama kutumia siku mbili za mkutano huo kujadili masuala yenye tija yatakayosaidia kuimarisha chama hicho na kuongeza manufaa yake kwa watumishi.
Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Lush Garden jijini Arusha.



