Wawa aiponza Singida FG

KLABU ya Singida Fountain Gate FC sasa haitaweza kusajili mchezaji mpya mpaka itakapomlipa aliyekuwa beki wa timu hiyo, Pascal Wawa baada ya nyota huyo raia wa Ivory Coast kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) imeeleza uamuzi huo umetolewa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Wawa alifungua kesi FIFA akidai malipo ya ada ya usajili na malimbikizo ya mishahara, hata hivyo Singida ikitakiwa kumlipa mchezaji huyo ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hiyo.
“Wakati FIFA imeifungia klabu hiyo kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeifungia kufanya uhamisho wa ndani.” Imeeleza taarifa ya TFF.



