Wawili wakutwa na virusi vya homa ya nyani

WIZARA ya Afya imesema watu wawili wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Homa ya nyani nchini.

Taarifa ya Waziri wa Afya Jenista Mhagama jana ilisema wizara ilipokea taarifa za wahisiwa hivyo kuchukua sampuli na kupelekwa maabara kwa ajili ya upimaji na vipimo.

“Uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox. Hadi kufikia sasa jumla ya wahisiwa wawili wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini,” ilieleza taarifa ya Jenista.

Ilieleza kuwa mmoja wa wagonjwa waliothibitika ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ilisema Machi 7, mwaka huu Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili.

Jenista alieleza kuwa dalili hizo ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo.

Aidha, serikali imesema kupitia Wizara ya Afya imejipanga kudhibiti ugonjwa huu na kuwahakikishia wananchi kuwa itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote.

“Wizara kwa kushirikana na Ofisi ya Rais Tamisemi na vituo vyote vya kutolea huduma za afya, inaendelea na ufuatiliaji uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki,” ilieleza taarifa ya Jenista.

Aidha, wizara imewataka wananchi wachukue tahadhari na wazingatie afua za kujikinga na ugonjwa kwa kuwa magonjwa ya virusi hayana tiba mahususi.

Wizara imewataka wananchi kuwahi kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi na matibabu wanapohisi dalili za ugonjwa wa homa ya nyani.

Pia, imewataka wananchi kuepuka kugusana, kupeana mikono kukumbatiana au kujamiiana na mwenye dalili za ugonjwa wa homa ya nyani.

Katika hatua nyingine, wizara imesema mpaka sasa mwenendo wa udhibiti wa ugonjwa wa Marburg upo vizuri na hakuna mgonjwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button