Wazazi Kigoma wakumbushwa malezi watoto wa kike

KIGOMA: Wazazi na walezi mkoani Kigoma wametakiwa kusimamia elimu, malezi na ndoto za watoto wa kike badala ya kuwapeleka kwenye ndoa za utotoni kwa watu wenye umri mkubwa sawa na baba au babu zao kwa lengo la kupata mali.
Kaimu Afisa Elimu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Fausta Akaro, alisema hayo akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, katika maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Mtoto wa Kike yaliyofanyika kimkoa katika Shule ya Msingi Gungu, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Katika hotuba yake, Rugwa alizitaka mamlaka na wadau mbalimbali mkoani Kigoma kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vinavyoweza kuharibu ndoto zao za maisha ya baadaye, ikiwemo ndoa za utotoni.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wazazi kusimamia elimu, malezi na matunzo ya watoto kwa usawa, akisema watoto wa kike hawapaswi kupewa nafasi ndogo huku watoto wa kiume wakipewa upendeleo kwa kuzingatia mtazamo kwamba watoto wa kike ni wa kuolewa tu.
Rugwa alisema Serikali itaendelea kusimamia sera, sheria na miongozo inayolinda na kusimamia masuala ya watoto, ikiwemo kupinga ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikivuruga na kupoteza ndoto za watoto wa kike.

Aliwaonya wazazi kutouza utu wa watoto wao kwa tamaa ya mali, akisisitiza kuwa watoto wa kike wanapaswa kupewa fursa ya kupata elimu na kutimiza ndoto zao.
Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Amina Kaniki, alisema maadhimisho hayo yanafanyika kwa lengo la kutafakari na kuchukua hatua kuhusu ulinzi na malezi ya watoto wa kike, pamoja na kuondokana na mila na desturi zinazowakandamiza.



