Wazazi wa wanafunzi 191 watoro kusakwa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imejipanga kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua wazazi wa wanafunzi 191 ambao hawajafanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili kwa sababu za utoro.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamuhuri William aliweka wazi hatua hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baada ya kumalizika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.

Alisema msako huo utaendeshwa nyumba kwa nyumba na utawarudisha shule wanafunzi watoro kwani wanarudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha kila mwanafunzi anafanikiwa kupata elimu msingi.

Alielekeza ofisi ya mkurugenzi, ofisa elimu, watendaji wa vijiji na kata kushirikiana kufanya tathmini ya utoro kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ili kubaini ukubwa wa tatizo na kuja na suluhisho kukomesha utoro.

Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo, Patrick Atanas alitaja sababu kuu za wanafunzi kutofanya mitihani ni mimba za utotoni, mwamko mdogo wa wazazi kuhusu elimu, shughuli za migodini, ufugaji na kilimo.

Alibainisha kwa mwaka huu wa masomo (2022/2023), halmashauri iliandikisha wanafunzi 2,157 wa kidato cha pili kwa ajili ya kufanya mtihani wa taifa katika shule 12 zilizosajiliwa na kwamba kati yao wanafunzi 191 hawajafanya mtihani huo.

“Kuna wazazi wanatamani watoto wafeli ili wasiendelee na shule, upande mwingine wanafunzi ndio wana shida, wenyewe hawapendi kusoma. Sisi kama idara ya elimu tunajitahidi kuwaelimisha waone umuhimu wa masomo,” alisema.

Alikiri kupokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya na kuahidi kushirikiana na mamlaka zote kupambana na utoro usio rasmi unaohatarisha na kurudisha nyuma maendeleo ya sekta ya elimu kwenye halmashauri hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button