Wazazi watakiwa kuchunga watoto wao

WAZAZI na walezi wametakiwa kufutilia mienendo ya watoto wao kubaini kama wamejiingiza katika wimbi la matumizi ya dawa za kulevya au madhara mengine.

Ofisa Elimu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini, Shabani Miraji ametoa wito huo leo Oktoba 18, alipozungumza na wazazi, walezi na wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari Namanga iliyopo wilayani Longido mkoani Arusha.

SOMA: DCEA yatoa mafunzo Arusha

Advertisement

Amesema wazazi na walezi wakifuatilia mienendo ya watoto wao watabaini viashiria ambavyo vinaweza kudhibitiwa mapema ikiwemo kuwahusia juu ya kutojiingiza kwenye makundi yasiyokuwa na tija.

Amesema DCEA kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetoa elimu kinga dhidi ya tatizo la dawa za kulevya kwa wanafunzi 405 wa Shule ya Msingi Namanga na wanafunzi 803 wa Shule ya Sekondari ya Namanga katika eneo la mpaka, kata ya Namanga wilayani Longido mkoani Arusha.

Wanafunzi hao walihamasishwa wakatae dawa za kulevya ili kutimiza ndoto zao za kielimu. Pia, walihimizwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga namba ya simu ya bure ya 119.