Waziri Gwajima atia mguu sakata mabinti wa chuo
DAR ES SALAAM; WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima ameingilia kati suala la video fupi inayosambaa mtandaoni ikiwaonesha mabinti wanaodaiwa kuwa ni wanafunzi wakishirikiana kumdhalilisha mwenzao kwa maneno na vipigo.
“Usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka tarehe 20.4. 2025 nilipokea tags nyingi kupitia mtandao wa Instagram wakinitumia video kadhaa zinazoonesha mabinti kadhaa wakishirikiana kumdhalilisha binti mwingine kwa maneno na vipigo na mambo mengine mabaya ambapo, watoa taarifa walidai kuwa, mabinti hao wote ni wanafunzi wa vyuo vikuu viwili tofauti nchini huku wengine wakidaiwa kuwa, wanasoma darasa moja na huyo binti wanayemdhalilisha na kumrekodi.
“Aidha, kwenye mazungumzo yao kama yanavyosikika, inaonekana ni ugomvi wa kumgombania mwanaume anayetajwa kwa jina moja la Mwijaku.
“Binafsi, nimesikitishwa sana kusikia mabinti wasomi ambao, wangetakiwa kujikita kwenye elimu na kuunganisha nguvu kupambana kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto badala yake wanatumia nguvu zao na elimu zao kukatiliana, kudhalilishana na kujidhalilisha wao kwa wao.
“
Udhalilishaji waliofanya kwa binti mwenzao haukubaliki kabisa na unastahili kukemewa kwa nguvu zote, kwani ni kinyume na sheria zote na pia siyo utu wala siyo haiba ya mwanamke wa Dunia ya sasa kwamba, akipishana jambo na mwanamke mwenzie au mtu yeyote, basi amfanyie udhalilishaji kwani, huko ni kujidhalilisha yeye mwenyewe na kudhalilisha wanawake wote,” amesema Dk Gwajima na kuongeza:
“ Nimewasiliana na manusura na kumuunganisha na huduma za ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia na huduma za Dawati la Jinsia Polisi ambapo, pia atapata Msaada wa kisheria ili haki itendeke.
“Nawasiliana na Wakuu wa Vyuo husika kupitia Madawati ya Jinsia kwenye Vyuo husika Ili hatua za nidhamu zichukuliwe.
“Nawasiliana na Waziri mwenye Dhamana na Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa hatua zaidi.”



