Waziri Kabudi ateua wajumbe Bodi TSN

DAR ES SALAAM; WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amefanya uteuzi wa wajumbe sita wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo imeeleza kuwa wajumbe hao wataungana na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Said Mwema aliyeteuliwa awali na Rais Samia Suluhu Hassan.

Wajumbe hao ni Dk Chisuligwe Khadudu, ambaye ni Mkufunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Joseline Kamuhanda Mkuu wa Kitengo cha Masoko Benki ya CRDB na Dk Ayoub Ryoba ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
“Elimbora Muro Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani wa kilichokuwa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Deogratius Kwiyukwa, alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Masoko kwenye Benki ya Biashara Tanzania (TCB) na Zamaradi Kawawa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,” imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa uteuzi huo umeanza Julai 22, 2025.



