Waziri Kairuki aja na vipaumbele 8 utalii

DODOMA. WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, amewasilisha bungeni bajeti ya wizara hiyo yenye vipaumbele 8.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake mwaka wa Fedha 2024/2025, amesema wizara itatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele hivyo, ambapo imeomba iidhinishiwe Sh 348,125,419,000.

Waziri Kairuki ametaja miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi ikiwa ni mwendelezo wa programu maalum ya Tanzania – t h e R o y al T o u r na filamu ya Amazing Tanzania.
Mikakati mingine ni kutangaza utalii kupitia matangazo katika ligi kuu za michezo mashuhuri duniani, matangazo kwenye ndege; misafara ya utangazaji utalii; matamasha makubwa ya kimataifa na mitandao mbalimbali ya kimataifa na vyombo vya habari;

“Kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo maeneo ya malikale pamoja na utalii wa fukwe, mikutano na matukio, meli, michezo, tiba na utamaduni.

“Kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi ili kuwezesha shughuli za utalii kufanyika.
“Kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale.

“Kuendelea kutekeleza mipango na mikakati ya uhifadhi pamoja na kuongeza kiwango cha uzalishaji na thamani ya mazao ya misitu na nyuki;

“Kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, misitu, ufugaji nyuki na malikale.

“Kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu mbalimbali na kufanya tafiti za kimkakati na kutoa huduma za ushauri zinazohusu masuala ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori, misitu na nyuki, malikale na uendelezaji utalii; na

“Kutekeleza mikakati ya kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi na mifumo ya ukusanyaji wa mapato na fedha za kigeni,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button