Waziri Mkuu apongeza uongozi mpya TEC

Rais TEC Mhashamu Wolfgang Pisa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa pongezi za dhati kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa kupata safu mpya ya uongozi wa Rais, Makamu wa Rais, Katibu na Naibu Katibu kwenye uchaguzi uliofanyika Juni 21, 2024.

Majaliwa amesema serikali inawaahidi viongozi hao kuwa itaendelea kutoa ushirikiano kwa Baraza hilo ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kiroho na kijamii kikamilifu kwa ustawi wa Kanisa Katoliki na Taifa kwa ujumla.

“Mungu awabariki viongozi wote na kuwasimamia katika majukumu yenu” amesema Waziri Mkuu.

Advertisement

Amesema kuwa kukamilika kwa safu hiyo ya uongozi ndani ya Kanisa Katoliki ni ishara kwamba kanisa linaendelea kujipambanua juu ya umuhimu wa ngazi za maamuzi zinazosaidia uratibu na usimamizi wa Kanisa.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Mhashamu Wolfgang Pisa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi (Rais), Mhashamu Eusebius Nzigilwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda (Makamu wa Rais), Padre Charles Kitima wa Jimbo Katoliki la Singida (Katibu Mkuu) na Padre Chesco Msaga wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu(Naibu Katibu).