Waziri Ndaki ataka halmashauri kutenga maeneo ya wafugaji

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili kukuza sekta hiyo na kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi.

Waziri Ndaki amebainisha hayo katika ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji katika vijiji vya Tanga na Njiwa. Amesema serikali ina nia nzuri ya kuendeleza sekta ya mifugo na kuzitaka halmashauri hizo na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo hilo.

Aidha, amewataka wafugaji kutolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Advertisement

Amesema serikali imeelekeza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kuanzia ngazi ya kijiji ambayo hayajasajiliwa, yanatakiwa kutambuliwa rasmi na kusajiliwa pamoja na kulindwa na kuhakikisha yanatumika kama ilivyopangwa kwa ajili ya kulishia mifugo pekee pamoja na kuwataka wafugaji kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.

Aidha amewataka wafugaji kufuatialia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kuwa taarifa zinazoonesha kumekuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili mwaka 2022 hali ambayo inatishia upungufu wa malisho ya mifugo pamoja na maji.