Wella : Mradi wa Kiloleni ukamilike Desemba

MKUU wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amewaagiza wasimamizi wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Msingi Kiloleni, iliyopo Kata ya Mapambano, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Agizo hilo amelitoa jana wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, ambapo alionesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji. Wella amesema ujenzi huo unatakiwa ukamilike kufikia Desemba mwaka huu ili Januari 2026 shule iweze kupokea wanafunzi kama ilivyopangwa.
Ametoa angalizo kuwa endapo mradi utacheleweshwa bila sababu za msingi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora itachukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wanaosababisha kuchelewa kukamilika kwa mradi huo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), unaotekelezwa kwa fedha za ndani, Kaimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiloleni, Teddy Michael, amesema kiasi cha Sh milioni 342.9 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa madarasa mapya, matundu ya vyoo, jengo la utawala, kichomea taka amoja na jengo la elimu ya awali. SOMA: Takukuru yabaini madudu ujenzi wa shule Geita



