Wengine 3 kortini jengo la Kariakoo

DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapandisha kizimbani wafanyabiashara wengine watatu wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa jengo la Kariakoo wakikabiliwa na mashitaka 31 ya kuua bila kukusudia kinyume cha sheria.

Washitakiwa hao ni mkazi wa Mbezi Beach, Sosteri Nziku (55), Aloyce Sangawe (59) na Stephen Nziku (28).

Wanaungana na wengine waliokwishafikishwa mahakamani ambao ni mkazi wa Mbezi Beach, Leondela Mdete (49), mkazi wa Kariakoo, Zenab Islam (61) na mkazi wa Ilala, Ashour Awadh (38).

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na wakili wa serikali, Roida Mwakamele mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Geofrey Mhini.

Awali, Roida aliiomba mahakama kubadili hati ya mashitaka kutokana na kuongezeka kwa washitakiwa katika shauri hilo.

“Tunaomba kubadili hati ya mashitaka kwani hapo awali hati hiyo ilikuwa na washitakiwa watatu na leo wameongezeka wengine watatu, hivyo kufikia idadi ya washitakiwa sita watakaoungana kwenye hati moja,” alidai Roida.

Hakimu Mhini alikubaliana na ombi hilo la kubadilishwa kwa hati hiyo.

Akiwasomea mashitaka yao, Roida alidai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kuua bila kukusudia.

Alidai kuwa Novemba 16, 2024 maeneo ya Mchikichi na Congo, Kariakoo Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam, isivyo halali washitakiwa hao walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31.

Waliopoteza maisha ni Said Juma, Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu, Rashid Yusuph na wengine 21.

Baada ya kuwasomea mashitaka, hakimu Mhini alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Aliwasomea washitakiwa masharti ya dhamana kuwa ni kuwa na wadhamini wawili na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kila mshitakiwa awe na Kitambulisho cha Taifa na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa watakaosaini bondi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja.

Wakili Roida alidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti hayo na kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 10, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button