Wenye visima ruksa kusambaza maji Dar

WAKATI Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), ikitoa ratiba ya mgao wa maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametembelea eneo la matengenezo ya bomba kubwa la inchi 72 katika kata ya Wazo, jijini Dar es Salaam, ambalo ni sehemu ya kimkakati ya kuongeza msukumo wa maji.
Katika ziara hiyo, Aweso ameagiza kuruhusiwa kwa wenye visima binafsi kuhudumia wananchi.
Akitoa tamko hilo leo Oktoba 27, 2022, amesema serikali imeruhusu matumizi ya maji ya visima binafsi na vya umma. ili vitumiwe na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi bila kikwazo chochote, hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
“Wenye visima binafsi toeni huduma sasa, ili wananchi wasiteseke na huduma hii,” amesema.
Ameiagiza DAWASA kuhakikisha ratiba ya mgao wa maji inasimamiwa na kufuatwa kikamilifu kama ilivyopangwa.
“Pasitokee janjajanja yoyote itakayosababisha lawama au upendeleo,” ameonya.
Amesema serikali ina mipango ya muda mfupi, ikiwemo kuanza kutumia maji ya mradi wa Maji Kigamboni ambao utawashwa Oktoba 30, ambao unatarajia kuzalisha takribani lita milioni 70 za maji ambazo zitasambazwa Kigamboni na maeneo ya katikati ya jiji.