WHI yaagizwa kutoa elimu ya huduma zao

DAR ES SALAAM: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ametoa wito kwa ‘Watumishi House Investments’ kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika ziara yake ofisi za taasisi hiyo, Kikwete amesema katika dunia ya sasa vijana ndio kundi kubwa linalokabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo ni muhimu taasisi hiyo kuwafikia kwa kampeni madhubuti za uelimishaji na utoaji wa taarifa sahihi.

Aidha, Waziri Kikwete amesema dhamira kuu ya ‘Watumishi House Investments’ ni kuhakikisha watumishi wanapata makazi bora na ya gharama nafuu, hata pale wanapohamishiwa maeneo ya mbali, ili kujenga mazingira rafiki yanayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali inalenga kujenga nyumba milioni 1, hivyo amewataka watumishi kuongeza kasi, ubunifu na kufanya utafiti katika kutafsiri maono ya Rais.

Waziri pia amesisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kujitegemea kifedha kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea bajeti kutoka serikalini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi House Investments, Sephania Solomoni, amesema taasisi imeanzisha mpango kazi mpya ukiwemo Faida Fund, mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaowawezesha wananchi kuwekeza kidogo kidogo na kunufaika na miradi ya makazi.

Amesema mfuko huo kwa sasa una thamani ya Sh bilioni 49, na kwamba taasisi inatarajia kuanza ujenzi wa nyumba 221 ndani ya mwaka huu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button