Wizara 14 zimeshahamia Mji wa Serikali Mtumba

UJENZI wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma umefikia wastani wa asilimia 93 na tayari wizara 14 zimeshahamia katika mji huo na zinatoa huduma kwa umma kutoka hapo.
Akizungumzia ujenzi wa mji huo jijini hapa, Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu wa Ujenzi wa Mji wa Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Omar Llyas amesema baadhi ya majengo yamefikia asilimia zaidi ya 67 mengine yamefikia hadi 100.
Kutokana na kufikia wastani huo wa ujenzi, wizara 14 zimehamia na watumishi wake wanatoa huduma kutoka katika mji huo, japokuwa majengo yao hayajakamilika kwa asilimia 100.
SOMA: Majaliwa atoa maagizo Mji wa Serikali
Wizara ambazo zimeshahamia ni Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji, Wizara ya Madini, Wizara ya Nishati, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya na Mambo ya Ndani ya Nchi.
Nyingine ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Katiba na Sheria.
Majengo yaliyopo katika mji wa serikali awamu ya kwanza ni 23 ya kawaida, awamu ya pili yamejengwa maghorofa ambayo yanajengwa kwa awamu ya kwanza hadi ya tatu, isipokuwa jengo la Wizara ya Fedha ambalo limekamilisha awamu zote tatu.
Katika mji huo majengo yaliyopo yana uwezo wa kuchukua watumishi 300, 500 na 1,400 na yapo majengo ya taasisi yenye uwezo wa kuchukua watumishi 150.
“Majengo ya wizara yenye ukubwa wa kuchukua watumishi 300 idadi yake yapo tisa, ya kuchukua watumishi 500 yapo 10, yenye kuchukua watumishi 1,400 yapo majengo matano,” amesema.
Mji huo wa serikali una eneo la ekari 6,000, kati yake ekari 1,500 zimejengwa ofisi hizo na eneo lililobaki ni kati ya mji huo na Ikulu ambalo lina ukubwa wa ekari 4,500 litatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa viwanja vya michezo na burudani.
Mji wa serikali una miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa zaidi ya 54 na pia kuna miundombinu mingine ambayo kwa sasa ipo juu ya ardhi, lakini mpango wa baadaye ni miundombinu yote kuweka chini ya ardhi.
Llyas amesema mji huo pia una eneo lenye viwanja 64 vya mabalozi vyenye ukubwa wa ekari kuanzia mbili na nusu hadi ekari saba na kuwa baadhi ya nchi kama China ina ekari 15 na Marekani ekari 50.
Amesema pia katika mji huo kuna eneo la ekari 33 ujenzi wa majengo ya Serikali ya Zanzibar pamoja na maeneo ya wazi kwa ajili ya shughuli nyingine za serikali na watumishi kwa ujumla pamoja na taasisi mbalimbali kujenga majengo yake.
Kutokana na ubora wa mji huo, amesema taasisi zaidi ya 70 zikiwemo za kifedha zimeomba kujenga majengo yao.
“Taasisi 70 zimeomba kwa waziri mkuu kujenga majengo katika mji wa serikali na bado yanafanyiwa kazi,” amesema.
Mji wa serikali unatokana na uamuzi wa TANU mwaka 1972 kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma na sheria yake ikaanza kazi 1973 ambapo Rais John Magufuli alitekeleza uamuzi huo.
Mwaka 2017 uamuzi huo ulianza, lakini ilipangwa eneo la Medeli ambalo lilionekana dogo na hivyo likatafutwa eneo hilo la Mtumba na kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza.
Ujenzi wa mji huo unazingatia Mpango Mkakati wa Jiji la Dodoma wa 2019-2039 kwa ajili ya uwekezaji miundombinu pamoja na ukijanishaji wa eneo hilo.




Freedom to work whenever I want — that’s what I love! I made $18,542 in a month doing this online. Check the details ———————⊃⫸ https://dailycash21.blogspot.com/