Wizara kupima ardhi yote, migogoro basi

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imelihakikishia Bunge kwamba imejipanga kumaliza migogoro ya ardhi na kutozalisha migogoro mipya kwa kupima ardhi yote nchini.

Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara yake bungeni jana, Waziri Dk Angeline Mabula alisema kupitia mradi huo, wizara hiyo imejipanga kumaliza migogoro ya ardhi nchini kwa kupima maeneo yote kwa haraka zaidi.

“Wizara haitazalisha migogoro mipya, badala yake itahakikisha inamaliza migogoro ya ardhi nchini ambayo mingi ni ya muda mrefu,” alisema Dk Mabula.

Alisema wizara kwa kutumia mkopo wa Dola za Marekani milioni 150 sawa na Sh bilioni 345 kutoka Benki ya Dunia utatumika katika kuondoa upungufu wa miundombinu ya upimaji, ya mfumo wa kielektroniki, uboreshaji makazi na upungufu wa majengo ya ofisi za ardhi za mikoa na hasa unalenga kuongeza kasi ya upimaji ardhi.

Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi na kuleta mageuzi makubwa kwenye wizara hiyo na kuwa kwa asilimia 100 mageuzi makubwa yanayoendelea katika wizara hiyo ni nguvu ya Rais.

Alisema migogoro mingi ya ardhi ni ya muda mrefu, lakini yote inaanzia katika ngazi za chini kwani watendaji mbalimbali wanaacha inaendelea kukua, kama ingekuwa inatatuliwa katika ngazi za chini isingefika bungeni.

Katika kuondoa migogoro hiyo, Rais Samia aliridhia ekari 2,385,326 zilizokuwa zikigombaniwa na wananchi wapewe jambo ambalo limesaidia kupunguza migogoro katika maeneo mbalimbali nchini.

Aliwataka wananchi katika maeneo ambayo tayari serikali imetenga na kuweka alama wasiingie kwani wanakuwa wanafanya kosa la kijinai na hivyo wafuate sheria bila shuruti.

Kuhusu mradi wa Benki ya Dunia, alisema unalenga kuongeza kasi ya upimaji ardhi, ni kutokana na wizara kukaa miaka yote tangu Uhuru na kufikia vijiji 12,318, lakini vijiji 10,000 vimepimwa na kati ya hivyo ni vijiji 2,680 ndivyo vyenye mpango wa matumizi ya ardhi, hivyo wizara inaona kuna haja kuwa na miundombinu kurahisisha upimaji.

Habari Zifananazo

Back to top button