Wizara ya Elimu yapokea vyuo kumi vya ufundi

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi amepokea Vyuo kumi vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Desemba 04 jijini Dar es Salaam katika Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho cha Yombo kati ya Naibu Katibu Mkuu huyo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Zuhura Yunus.
Akizungumza baada ya kupokea vyuo hivyo Prof. Mushi amesema Wizara imevipokea vyuo hivyo na ina uwezo wa kuvilea kuhakikisha vinatoa mafunzo yenye tija kwa walengwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Wizara itaboresha mindombinu ya vyuo hivyo pamoja na kumalizia ujenzi kwa baadhi ya Vyuo.
“Mhe. Rais ametoa fedha nyingi kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hivyo tutaboresha mazingira ya vyuo vyote kumi ikiwemo na kukamilisha ujenzi” amesema Prof. Mushi.
Aidha ameongeza kuwa kazi kubwa ya Wizara ya Elimu ni kuongeza fursa kwa kuhakikisha kuna miundombinu ya kutosha, kusimamia ubora wa elimu kwa kuwa na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoa mafunzo kwa walimu kazini.
Naye Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus amesema kuwa hatua ya kukabidhi vyuo hivyo kwa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni utekelezaji wa agizo la Dk Samia Suluhu Hassan alilotoa Aprili, 2024.
Ameeleza kuwa katika agizo hilo Rais aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kubaki na jukumu la kuratibu masuala ya watu wenye ulemavu na suala la kutoa mafunzo stadi yaelekezwe kwa Wizara ya Elimu.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu kutika Ofisi ya Waziri Mkuu, Radheed Maftah amewaambia viongozi hao kuwa katika vyuo kumi vinavyokabidhiwa, vitano vipo hai na vinaendelea kutoa mafunzo, vinne vinaendelea na ujenzi na kimoja kinahitaji maboresho makubwa ya miundombinu.