Wizara yawasilisha taarifa yake kamati ya bunge

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilisha na kujadili taarifa ya utekelezaji majukumu yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Utalii.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji taarifa ya utekelezaji mbele ya Kamati hiyo leo tarehe 12 Machi 2023 jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, DkAngeline Mabula ameeleza maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayofanywa na wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara ya Ardhi.

Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii kwa sasa inaoongozwa na Mbunge wa Jimbo la Korogwe, Timotheo Mzava huku makamu mwenyekiti wake ni Mbunge wa jimbo la Kondoa Ally Juma Makoa ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Akizumgumza kwa mara ya kwanza kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii Timotheo Mzava amewataka wajumbe wa kamati pamoja na wizara kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu ya kamati ili kufanikisha kazi na kusisitiza kuwa, ushirikiano ndiyo njia bora ya kuja na matokeo chanya.

Kupitia kamati hiyo, Waziri Mabula alieleza miradi inayotekelezwa na wizara yake kuwa ni pamoja na ule wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK), program inayotekelezwa wilayani Meru Mkoa wa Arusha, mradi wa ujenzi wa soko la Madini ya Tanzanite ulioko Mererani unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na kazi ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la Namanga.

Kamati hiyo ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii inatarajiwa kutembelea miradi inayotekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia siku ya jumatano tarehe 15 hadi 18 Machi 2023 mkoani Arusha kabla ya Wizara hiyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Mpango wa Bajeti (RANDAMA) kwa mwaka wa fedha 2023/2024

Habari Zifananazo

Back to top button