Yanga mguu sawa Afrika Kusini

MENEJA wa Yanga, Walter Harrison amesema maandalizi yao kuelekea mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la soka Afrika (CAF) dhidi ya Marumo Gallants yanaendelea vizuri na wachezaji wote wapo katika hali nzuri.

Yanga iliwasili katika mji wa Rustenburg, Afrika Kusini juzi mchana na kulakiwa na Balozi wa Tanzania, Gaudence Milanzi na Watanzania waishio nchini humo wakiwemo mashabiki wa watani zao Simba.

Akizungumza na waandishi wa habari meneja huyo alisema kikosi chao kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye uwanja unaomilikiwa na hoteli waliyofikia na leo jioni ndio watakwenda kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Royal Bafokeng utakaochezewa mechi hiyo.

“Wachezaji wote tuliokuja nao wapo katika hali nzuri kiafya na benchi letu la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi linaendelea na ratiba yake kama kawaida ya kuiandaa timu kuhakikisha tunapata kile kilichotuleta huku,” alisema Walter.

Kwa mujibu wa Walter, Nabi amekuwa akizungumza na wachezaji akimtaka kila atakayepata nafasi kucheza kwa jihadi na kujituma kwa nguvu zake zote kama walivyofanya kwenye mchezo wa kwanza.

“Tunatakiwa kuipigania heshima ya klabu yetu kwa kucheza kama wanajeshi, tunatakiwa kwenda kuipigania Yanga, tunatakiwa kwenda kuipigania Tanzania, natamani kuona kila mchezaji akicheza kwa jihadi na kujitolea nguvu zake zote,” alisema Nabi.

Katika mchezo huo, Yanga inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kutinga fainali ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika, hiyo ni baada ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam wiki iliyopita.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button