Yanga nguvu kwa mashabiki vita ya kutetea ubingwa Bara

DAR ES SALAAM – KLABU ya Yanga imesema inategemea nguvu ya mashabiki kushinda michezo yote iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ili kutetea taji hilo.
Hayo yalielezwa Dar es Salaam na Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe wakati wa maandalizi ya safari yao kuwafuata Fountain Gate kwa ajili ya mchezo utakaochezwa Jumatatu.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa pointi 67 baada ya kucheza mechi 25, zikisalia mechi tano kukamilisha ligi ikiwa ni pamoja na mchezo wao dhidi ya Simba ulioahirishwa mwezi uliopita.
Kamwe alisema wanahitaji kuungwa mkono na mashabiki wao kila kona ya nchi wakati huu kukamilisha mechi zilizosalia kwa kishindo na kushinda ubingwa.
“Yanga inakuomba wewe shabiki na mwanachama kutuunga mkono popote tutakapoenda wakati huu wa mwisho wa ligi ili tufunge hesabu vizuri,” alisema Kamwe.
Aliongeza: “Tunafahamu tuna mashabiki wengi Manyara, Arusha pamoja na mikoa mingine yote, tunahitaji nguvu ya pamoja kama Yanga kutoka kwenu, sasa hivi tupo katika nyakati za kufunga mahesabu twendeni kikubwa na kikatili zaidi tukamalize msimu kwa furaha”.
Kamwe alisema katika mechi hiyo atakosekana Yao Kouassi ambaye bado hajapona vizuri majeraha yake na kueleza kuwa wataikosa huduma yake kwenye michezo yote iliyosalia msimu huu, lakini Pacome Zouzoua na Khalid Aucho wanatarajiwa kuwa timamu baada ya wiki mbili.



