Yanga, Singida Black Stars hapatoshi

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa Yanga kuikaribisha Singida BS Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam na Fountain Gate kuivaa Tabora United, Uwanja wa Tanzanite Babati, Manyara.

Kwenye michezo iliyopita Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya KMC huku Singida BS ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi alisema, “Tumejiandaa kama ambavyo tulijiandaa mchezo uliopita. Tunafahamu ni mchezo mgumu na muhimu hivyo tumeongeza umakini mkubwa kwani mpango wetu ni kucheza kwa umakini zaidi.

“Tunafahamu Singida ni timu nzuri sana ina wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, lakini ni matumaini kuwa tutakuwa na mchezo mzuri uwanjani,” alisema Hamdi.

Alisema ataangalia vitu gani anapaswa kubadilisha kwenye kikosi kwani katika mchezo dhidi ya JKT hawakucheza vizuri lakini Singida wao walishinda dhidi ya timu hiyo.

“Wanaonifahamu wanajua namna gani nina kuwa na uchu wa kupata ushindi, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba tunapaswa kuwaheshimu wapinzani kwani mpira ni mchezo wa ushindani na kila mtu anatumia mbinu mbalimbali kujaribu kushinda hivyo lazima niende kwa tahadhari na umakini hata kama nahitaji kupata alama tatu,” alisema Hamdi.

Kwa upande wake, Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma alisema wanaiheshimu Yanga kama moja ya timu bora katika soka la Tanzania lakini lengo lao ni kupata pointi tatu kwenye mchezo huo.

Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 49 kwenye michezo 19 na Singida Black Stars inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 37 baada ya michezo 19.

Katika mchezo wa Uwanja wa Tanzanite Manyara wenyeji Fountain Gate wanaingia kwenye mchezo wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa kwa mabao 3-0 na Kagera Sugar wakati Tabora United wao walitoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Kengold.

Tabora wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi 32 na Fountain wanashika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 21 baada ya kucheza michezo yote 19.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button