Yanga yatakiwa kugharamia uharibifu Uwanja wa Mkapa

DAR ES SALAAM: WIZARA ya Utamaduni Sanaa na michezo imewasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ikiwataka Yanga kugharamia uharibifu uliofanyika kwenye mchezo wao dhidi ya Al Ahly.

Barua rasmi iliyowasilishwa kwa TFF imeeleza kuwa: “Wizara ilitoa kibali cha kufanyika kwa mchezo wa kimataifa kati ya Yanga SC (Tanzania) dhidi ya Al-Ahly (Misri) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliofanyika tarehe 2 Desemba, 2023,”

“Hata hivyo, Wizara imepokea malalamiko kutoka kwa uongozi wa uwanja ambapo mashabiki wa klabu ya Yanga wanalalamikiwa kwa kuwasha fataki wakati mchezo ukiendelea na kusababisha vurugu zilizopelekea baadhi ya viti kung’olewa,”

Advertisement

“Wizara inakemea vikali kitendo hiki na kuwataka klabu ya yanga mara moja kuwasiliana na uongozi wa uwanja ili kuweza kubaini ukubwa wa tatizo na kuona namna bora ya kulitatua,”

“Kwa barua hii, Wizara inawasilisha rasmi malalamiko haya kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuwa ndiye mdhamini wa vilabu hivi kwa maombi ya matumizi ya uwanja huu ili kuwajulisha Klabu ya Yanga SC kuwa inapaswa kugharamia matengenezo ya viti vilivyong’olewa na mashabiki wakati wa mchezo huo,”