DODOMA: Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amezindua jengo la wodi ya wazazi Zahanati ya Kikuyu Kaskazini lililogharimu Sh milioni 84.
Jengo hilo limejengwa kutokana na fedha za mfuko wa jimbo na Halmasauri ya Jiji la Dodoma ambapo amelikabidhi kwa uongozi wa zahanati hiyo kwa ajili ya matumizi.
Pia, ametoa gari la wagonjwa (Ambulance) pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya vituo vya afya Dodoma Jiji.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mavunde amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa magari ya wagonjwa na vifaa tiba kwa vituo vya afya jijini Dodoma.
“Katika kuboresha mazingira ya zahanati hii nitahakikisha tunaanza ujenzi wa uzio mapema iwezekanavyo ili eneo letu liwe salama na lenye staha, moja jambo nitakalolifanya siku chache zijazo ni upatikanaji wa magari mengine mawili ya wagonjwa (ambulance), amesema.
Akitoa salamu zake, Mkuu wa Wilaya Dodoma Jabir Shekimweri amesema sekta ya afya Dodoma inaendelea kuimarika kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge Mavunde na hivyo kuwataka wataalamu wa afya kuboresha huduma kwa wananchi na kutunza vifaa vyote vilivyotolewa na kuhakikisha vinafanya kazi iliyokusudiwa.