Zaidi ya mil 400 kusambaza mitungi ya gesi Dodoma

CHAMWINO, Dodoma: MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa cha sh 406,712,250 kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhudumia Mkoa wa Dodoma kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo 6 pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji ambapo kwa mkoa huo
Mkuu wa Mkoa amebainisha hayo leo Januari 08 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ugawaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku iliyofanyika wilayani Chamwino mkoani Dodoma ambapo REA imeingia mkataba na kampuni ya Lake Gas Ltd kwaajili ya kutoa huduma hiyo.
Senyamule amefafanua kuwa, katika mkoa huo mitungi ya gesi itauzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 ambayo ni sawa na sh 20,825 kwa mtungi mmoja (kutoka bei ya sh 41,650).
Amesema Serikali kupitia REA inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wananchi wanaweza kumudu gharama za matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao, kutunza mazingira na kuboresha maisha yao.
SOMA: Mitungi ya gesi kutolewa bure vijijini
“Kupitia mradi huu, wananchi watafaidika na punguzo la bei ya gesi ya mitungi kwa asilimia 50 na watapata mafunzo ya jinsi ya kutumia nishati hiyo kwa usalama na unafuu,” ameongeza Senyamule.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu REA, Mha. Emanuel Yesaya amesema mradi huo umelenga kusambaza mitungi ya gesi 19,530 ya kilo 6 pamoja na vifaa vyake katika wilaya sita (6) za mkoa huo ambapo kila wilaya itapata jumla ya mitungi 3,255.
“Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini na pembezoni mwa miji,” amesema Mha. Yesaya
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja amesema mradi huo utapunguza ukataji wa miti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi, vifo vinavyosababishwa na kuvuta hewa chafu inayotokana na kuni na mkaa pamoja na kupunguza ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya familia.
Ameongeza kuwa, mradi huo utapunguza umaskini kwa kuwapa muda zaidi wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi pindi wanapotumia mitungi ya gesi kama njia mbadala ya kupikia badala ya kuni na mkaa.