Zaidi ya wananchi 10,000 wanufaika kambi ya upimaji

DAR ES SALAAM; WANANCHI zaidi ya 10,000 wamepatiwa matibabu bure katika kambi ya siku tatu ya upimaji wa afya na macho kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja,Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Alhaji Mohammedraza Dewji, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia ithninasher Mkoa wa Dar es Salaam iliyoandaa kambi hiyo amesema ni sehemu ya kutimiza mafunzo ya Imamu Hussein (AS) na kwamba kwa kiasi kikubwa yamevuka lengo.

“Kambi hii ni kumbukizi ya kifo cha mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS) na iligawanyika sehemu kuu mbili, moja ilikuwa kupata elimu juu ya Imam Hussein (AS) na nyingine ni utolewaji bure wa vipimo vya afya, dawa na kufanyiwa upasuaji wa macho,” amesema.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika mafunzo hayo ya afya mwaka huu, ni tofauti na mwaka jana kutokana awamu hii kuwa na mwitikio mkubwa wa watu wengi kujitokeza kupata huduma na matibabu.

Amesema zaidi ya watu 4800 walijitokeza kwenye upimaji wa macho na kwamba kati yao 289 walikutwa na changamoto za mtoto wa jicho na matatizo mengine na watapangiwa kufanyiwa upasuaji.

“Waliokutwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho wapatao 97 na walipelekwa kwenye Hospital ya Medwell iliyopo Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na wengine waliobakia, watapangiwa siku ya kwenda kupata matibabu na upasuaji,” amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema wapo baadhi ya wagonjwa hawakuwa tayari kwenfa kupatiwa matibabu Kibaha kutokana na umbali, hivyo watapangiwa kwenda hospitali ya Temeke Charitable Hospital na hawatatibiwa kwa gharama yoyote,

Amesema wagonjwa 2,817 walipewa miwani ya kusomea na wengine wapatao 1813 walipewa miwani ya kutembelea, huku 3500 walipewa dawa na kutibiwa matatizo ya macho.

Kuhusu kuchangia damu amesema walikusanya chupa za damu salama  229 kwa kushiriiana na mpango wa Taifa wa Damu Salama.

Mwenyekiti huyo amesema wanawake  427 walifanyiwa vipimo vya kansa ya shingo ya kizazi na waliokutwa na changamoto walitakiwa kufanyiwa vipimo zaidi.

Pia upande wa wanaume wapo waliofanyiwa vipimo vya teuzi dume na sita walikutwa na changamoto. Huku pia kukifanyika vipimo vya magonjwa yasyoambukiza.

Kwa upande wake daktari mkuu wa kambk hiyo,  Alhussein Molloo amesema kambi ilikuwa ya mafanikio na kwamba vipimo mbalimbali vilitumika kwa wagonjwa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button