Zelensky: Mali za Urusi Zitaifishwe

KIEV, UKRAINE : RAIS wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametoa wito kwa mataifa ya Magharibi kutaifisha mali zote za Urusi zilizozuiwa, akisema hatua hiyo itasaidia kuleta amani badala ya kuendeleza vita.
Zelensky ametoa wito huo Alhamisi kupitia njia ya mtandao wakati akihutubia mkutano wa Helsinki, ulioandaliwa kuadhimisha miaka 50 tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kihistoria kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti yaliyosaidia kumaliza Vita Baridi.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Zelensky amesema fedha na mali za Urusi zilizokamatwa zinapaswa kutumika kusaidia juhudi za amani na kuwasaidia waathirika wa uvamizi unaoendelea badala ya kuruhusiwa kuchochea vita zaidi. “Kutaifishwa kwa mali hizo kutaweza kusaidia kupunguza uchokozi wa Urusi,” alisema.
Katika maelezo yake, Zelensky aliongeza kuwa kuna haja ya kufanyika mabadiliko ya uongozi nchini Urusi, akisema kuwa Rais Vladimir Putin ameendelea kuwa chanzo cha machafuko na kuvuruga usalama wa mataifa jirani. SOMA : Marekani yakanusha kusitisha silaha Ukraine
Kauli hiyo imetolewa wakati mashambulizi mapya ya Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kiev, yameripotiwa kusababisha vifo vya takriban watu sita usiku wa kuamkia Alhamisi.
Mamlaka za Ukraine zimesema mashambulizi hayo yalihusisha makombora ya angani na kwamba idadi ya majeruhi bado inaendelea kuthibitishwa.