Ziara ya Rais Samia India yafungua fursa nchini

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kutokana na ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India iliyofanyika Novemba 9 -10 imefungua fursa mbalimbali katika sekta za uwekezaji ikiwemo kukutanisha kampuni ya nchi hizo mbili.
Waziri Mkumbo amesema hayo leo Disemba 6, 2023 jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kampuni ya Mahindra Tanzania ambayo itazalisha magari kwa miezi sita ijayo, kutokana na ushirikiano huo utasaidia vijana kupata ajira.
“Tumeikaribisha rasmi kampuni hii ya Mahindra, na leo nimekuja kuzindua uwepo wake hapa Tanzania ambayo itakuwa inauza magari yanayozalishwa na Mahindra hapa nchini, na hatua ya pili ndani ya miezi sita ijayo wataanza kuzalisha magari”. Amesema Waziri mkumbo”
Amesema juhudi za serikali zimesaidia kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kuendelea kufungua fursa mbalimbali za ajira.
Mkurugunzi Mtendaji wa Kampuni ya GF Trucks & Equipment Ltd, Imran Karmali amesema mwaka 2023 wamezalisha magari 1000 huku malengo yao ikiwa ni kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuongeza magari madogo huku akimpongeza Rais Samia kwa kundeleza ushirikiano baina ya Tanzania na India.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uwekezaji TIC, Gilead Teri ameipongeza kampuni hiyo na kwa miezi mitatu iliyopita kati ya mwezi Julai na Septemba takwimu zinaonesha kuwa uwekezaji umeingia kiwango cha Dola bilioni 1 ambayo ikiwa ni mara mbili ya kiwango cha miezi hiyo mwaka 2022.



