Ziara ya Samia India yaanza kulipa

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi Mambo ya Nje na Masuala ya Bunge wa India, Shri Muraleedharan amewataka wawekezaji kutoka India waiunganishe nchi hiyo kibiashara na Tanzania ili kukuza uchumi.

Muraleedharan amesema kupitia uwekezaji baina ya Tanzania na India, uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi miongoni mwa nchi za Afrika kwa kuwa India ni miongoni mwa nchi zenye uchumi imara duniani.

Muraleedharan alisema hayo Dar es Salaam jana wakati ujumbe wa wawekezaji kutoka India ulipokutana na Watanzania kwa lengo la kujadili fursa zilizopo nchini.

Advertisement

Ujumbe huo wa wawekezaji na wafanyabiashara nchini ni matunda ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India mwezi uliopita kutangaza vivutio vya kukuza uchumi.

Muraleedharan alisema ziara ya Rais Samia nchini India imekuwa na manufaa hasa walipokubaliana kufanya biashara kwa kutumia sarafu ya fedha za nchi hizo.

Alihimiza wadau wajitokeze kuimarisha fursa hiyo ili kuongeza kiwango cha biashara.

Muraleedharan alisema mazungumzo ya wafanyabiashara wa India na Tanzania yalifanikishwa na Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na India (TIBF) na ni muhimu wawekezaji wa India watumie fursa hiyo kuhamasisha biashara baina ya nchi hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis alisema Tanzania imejizatiti kushirikiana na India katika maeneo ya kukuza biashara.

Latifa alisema katika miaka kadhaa zipo sekta ambazo wamekuwa wakishirikiana ikiwamo masuala ya Tehama, usafirishaji wa bidhaa kwenda India na hata masuala ya fedha.

“Tantrade ni daraja la wafanyabiashara baina ya Tanzania na India na Tanzania kuna fursa mbalimbali hivyo wajitokeze kutumia majukwaa hayo kufikia masoko mbalimbali,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Rafael Maganga alisema ujumbe kutoka India ni matunda ya kazi ya Rais Samia.

Maganga alihimiza wawekezaji watambue kuwa Tanzania ni nchi yenye sera imara za biashara na uwekezaji sanjari na mazingira wezeshi katika masuala hayo.

Alisema Tanzania ina idadi ya watu milioni 68 hivyo ni soko kubwa na sekta binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi hivyo ushirikiano huo ni wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Wakati akiwa India, Rais Samia alisema Tanzania na nchi hiyo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kimkakati.

Alisema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi mjini New Delhi.
Alisema kupitia ziara hiyo, wanatarajia kufungua fursa zaidi za ushirikiano wa kimkakati kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Rais Samia alisema kwenye biashara takwimu zinaonesha hadi mwaka jana, thamani ya biashara kati ya Tanzania na India ilikuwa Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na Sh trilioni 7.77.
Alisema takwimu hizo zinaifanya India kuwa mshirika wa tatu mkubwa wa kibiashara wa Tanzania na mshirika wa tano mkubwa wa uwekezaji nchini.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *