Kishindo CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kampuni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Amani visiwani Zanzibar utakaofanyika Desemba 17, 2022.
Kampeni hizo zimezinduliwa jana Alhamisi, Desemba 1, 2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ambapo  pamoja na mambo mengine, amemnadi mgombea wa chama hicho, Abdul Yussuf Maalim.
Katika uzinduzi huo, Shaka amewataka wananchi wa jimbo hilo kuchagua mgombea iliyesimamishwa na CCM kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kuendeleza kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Amebainisha kuwa  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi anaendelea kufanya kazi kubwa na nzuri, hivyo anastahili kupewa viongozi atakaoshirikiana nao katika  kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha kasi ya kuwaletea maendeleo  iliyoanza inakamilishwa kulekea 2025 ili CCM iendelee kuaminiwa kwa kipindi kingine.
Aidha, amefafanua kuwa  kazi ya kuleta maendeleo hususan katika jimbo hilo haiwezi kuletwa na kila mtu, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kumchagua mgombea aliyesimamishwa na CCM ili atimize wajibu huo kwa watu wa jimbo hilo.
Kazi ya kuleta maendeleo ya nchi hii hapewi kila mtu, kazi ya kuleta maendeleo jimbo la Amani sio kila mmoja anaweza kuleta maendeleo, wapo wenye uwezo wa kuleta propaganda kwenye jimbo  la Amani ”
“Lakini wapo wenye uwezo wa kuleta maendeleo wana amani mkasema kweli haya ni maendeleo ambayo tunayahitajia, ndiyo maana tukasema Abdul songa mbele nenda ukapeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi nawahakikishia  ataifanya kazi hii kwa uweledi na ustadi wa hali juu” amesema Shaka
Awalinde,  Shaka aliwakumbusha wananchi juu ya  kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia na Rais Mwinyi katika kipindi cha miaka miwili ni kubwa, ya kutukuka na  hivyo wanastahili kupongezwa na kuungwa  mkono ikiwemo kumchagua mgombea huyo wa CCM ili kushirikiana katika kuwaletea wana Amani maendeleo.