Madini kupewa chapa ya ‘Made in Tanzania’

GEITA: MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imepanga kusimamia kampeni ya usajili na uwekaji wa chapa ya ‘Made in Tanzania’ katika madini yanayozalishwa nchini.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya matumizi ya chapa ya Made in Tanzania katika bidhaa zote zinazozalishwa nchini ikiwa ni sehemu ya utambulisho wa taifa nje ya nchi.

Meneja Ukuzaji Biashara wa TANTRADE, Deo Shayo ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza katika kongamano la Made in Tanzania katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini mjini Geita.
Amesema kusudi la TANTRADE ni kuona madini yanayozalishwa Tanzania yanatambulika kimataifa, kuipa nguvu chapa ya Tanzania, kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji.
“Tunakusudia kuwaambia wazalishaji na wafanyabiashara wa madini wajisikie fahari kuyauza yakiwa na ile chapa ya Made in Tanzania.

“Itakuwa ni jambo la aibu kama kuna wajanja wanafanya uzalishaji hapa harafu wanakubali kuuza madini nje ya nchi yakiwa na utambulisho wa nchi zingine”, amesema Deo.
Deo amesema madini adhimu ya Tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee pamoja na madini mengine yanayozalishwa kwa uwingi ni miongoni mwa madini yatakayopewa kipaumbele.
Aidha amewaomba wafanyabiashara kuchangamukia usajili wa bidhaa zao kwa chapa ya made in Tanzania kwani mpaka sasa takribani asilimia 85 ya huduma ya Tantrade zinatolewa mtandaoni.

Amesema kwa kipindi cha miezi 10 iliyopita takribani aina ya bidhaa 120 zimesajiliwa kwenye chapa ya taifa nah atua zaidi zinaendelea kuongeza mwamko na mwitikio katika kampeni hiyo.
“TANTRADE tutahakikisha tunaendelea kuwa mstari wa mbele tunatoa fursa za maonyesho kwa kila aliyejisajili na Made in Tanzania tunatangaza bidhaa zao kupitia Kanzi Data yetu.
“Pia TANTRADE itafungua kituo cha kimataifa cha biashara pale Ubungo, kwa kila aliyejisajili atapewa nafasi ya kutangaza sampuli ya bidhaa zake pale”, amesema Deo.



