JUMLA ya Wapiga Kura 114,647 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani Mkoa wa Mjini, Zanzibar na Kata saba za Tanzania Bara, kesho Desemba 17,2022.
Hayo yamesemwa leo Desemba 16, 2022 na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele katika risala ya uchaguzi huo mdogo ambapo vituo 289 vya kupigia kura vitatumika.
“Tume imekamilisha maandalizi muhimu ikiwemo usambazaji wa vifaa vya uchaguzi na mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi katika ngazi ya vituo vya kupigia kura” amesema Jaji Mwambegele.
Mwambegele amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya siasa na wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wa uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani, Mkoa wa Mjini, Zanzibar na Uchaguzi wa Udiwani katika Kata saba za Tanzania Bara.
Mbali na jimbo la Amani pia uchaguzi huo mdogo utashirikisha, Kata za Majohe (Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam), Mndumbwe ( Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba), Njombe Mjini (Halmashauri ya Mji wa Njombe), Dunda (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mwamalili (Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga), Mnyanjani ( Halmashauri ya Jiji la Tanga) na Vibaoni (Halmashauri ya Wilaya ya Handeni).
Aidha, Amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye majimbo na kata zinazofanya uchaguzi huo.
Mwambegele, amesema sheria na kanuni za uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.
Aidha, amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika jimbo ya Amani na Kata saba za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua Mbunge na madiwani wanaowataka.
Pia, amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zinamalizika leo jioni saa 12:00 hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.
Wakati huo huo Mwambegele amevikumbusha vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi wa huo kesho, kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura.
“Pili upigaji kura utafanyika katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
“Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni”amesema
Amesema watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Amani Wilaya ya Mjini Zanzibar ni wale tu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na wana kadi za mpiga kura.
Aidha Jaji wa Rufaa Mwambegele alisema kwa upande wa uchaguzi mdogo wa madiwani watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wana kadi zao za mpiga kura.
Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala ambavyo ni
Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Jumla ya vyama vya siasa 16 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo ambapo Tume imevipongeza vyama hivyo na wagombea wao kwa kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huu mdogo wa Ubunge na Udiwani.
Comments are closed.