Ni jasho na damu robo fainali FA

KUMEKUCHA robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) inaanza kutimua vumbi wikiendi hii, ambapo Singida Big Stars (SBS) inatarajiwa kuwakaribisha Mbeya City katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Liti, mkoani Singida leo.
Aidha, wanalambalamba wa Chamazi, Azam FC wanatarajiwa kuwakaribisha wakata miwa wa Manungu, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kesho.
Ni mchezo wa kutoana jasho kutokana na umuhimu wa kila mmoja kutaka ushindi ili kusonga mbele hatua ya nusu fainali na hata fainali na kuchukua taji ambalo litawapa uwakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
SBS vs Mbeya City Singida Big Stars ilitinga hatua hii baada ya kuwaondosha vinara wa Championship, JKT Tanzania kwa bao 1-0 mchezo uliochezwa mjini Singida. Mbeya City ilitinga hatua hii baada ya kuwaondosha Kagera Sugar kwa bao 1-0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Mchezo wa leo unazikutanisha timu mbili zenye kiwango tofauti, Singida Big Stars imekuwa ni bora msimu huu ikiwa imesheheni wachezaji wengi wa nje na wa ndani, ambao wameisaidia timu hiyo kuingia kwenye nne bora katika msimamo wa Ligi Kuu.
Katika michezo 25 iliyocheza Singida imeshinda 14, sare sita na kupoteza michezo mitano ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 48 ikikimbizana na Azam FC, ambao wako nafasi ya nne kwa pointi 47 tofauti ya pointi moja.
Singida Big Stars imefunga jumla ya mabao 29 na kuruhusu 20 kwenye nyavu zao ikionesha wazi ushindi wanaoshinda katika mechi zao nyingi ni wa mabao machache kuanzia bao 1-0 wakizidi kidogo ni mabao mawili au matatu.
Kikosi hicho kina wachezaji hatari kama Bruno Gomes anayeongoza kwa kufunga mabao tisa kwenye ligi na wengine wakihusika kama Meddie Kagere, Deus Kaseke, Kazengu Kazadi wote hao wakiwa na mchango kwa namna moja au nyingine na kuiwezesha timu kuwa katika kiwango bora.
Uzoefu wa wachezaji walionao unawapa jeuri chini ya kocha mzoefu, Hans Pluijm. Wana kila sababu ya kushinda mchezo huo kwa sababu ya ubora wa kikosi chao, watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani na mashabiki wao. Lakini hawapaswi kuwabeza wapinzani wao kwa sababu Mbeya City ni timu isiyotabirika na ngumu. Timu hii inaweza kushinda hata ikiwa ugenini kama ilivyo kwa Singida Big Stars.
Timu hii imefunga jumla ya mabao 29 ikifungwa 38 ikionesha wazi namna wanavyoruhusu mabao kwa wapinzani wao lakini pia, ni timu inayocheza kwa kushambulia na kwa tahadhari mara nyingi. Mchezaji wake, Sixtus Sabilo amekuwa katika kiwango bora akihusika kwa kufunga mabao tisa Ligi Kuu katika kikosi hicho.
Licha ya timu hiyo kutofanya vizuri sana kwenye ligi wamekuwa wakionesha ushindani hasa kwenye mechi za mashindano kama hizi. Timu hizi zimeshakutana mara mbili kwenye ligi na Singida iliondoka mbabe baada ya mchezo mmoja kushinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Liti na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Je, nani kuingia nusu fainali? Ni yule aliyejiandaa kimbinu dhidi ya mwenzake. Mshindi wa mchezo huu atacheza nusu fainali na mshindi wa mechi kati ya Yanga na Geita Gold FC. AZAM v MTIBWA Azam FC baada ya kukata tamaa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wameweka nguvu katika mashindano hayo hivyo kwa vyovyote watapambana kufa au kupona kuhakikisha wanapata ushindi.
Licha ya kuyumba kidogo tofauti na walivyoanza msimu huu bado wana nafasi ya kufanya vizuri kutokana na ubora wa kikosi chao unaoongozwa na Prince Dube, Kipre Junior, Abdul Sule- man ‘Sopu’ na wengine. Kwenye ligi Azam baada ya kucheza michezo 25, imeshinda 14, sare tano na kupoteza michezo sita ikiwa imekusanya pointi 47.
Imefunga jumla ya mabao 39 ikionesha wazi safu ya ushambuliaji iko vizuri na ina nafasi ya kufunga mabao kwa kila mchezo. Imeruhusu kufungwa mabao 25 ambayo sio mengi sana ila wanaonekana wanaweza kufungika wasipokuwa makini.
Timu hii ilitinga hatua hii baada ya kuwaondosha mabingwa wa Mkoa wa Mwanza, Mapinduzi FC kwa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Inakutana na Mtibwa ambao hawako vizuri sana wala vibaya.
Baada ya kufanya vibaya kwenye ligi takribani misimu miwili iliyopita wakinusurika kushuka daraja kwa sasa wameonekana kuna mabadiliko kidogo baada ya kuamua kusajili wachezaji hadi wa kimataifa kuonesha wazi wamedhamiria kufanya vizuri msimu huu. Takwimu zao za Ligi Kuu zinaonesha katika michezo 25, wameshinda saba, wamepata sare nane na kupoteza michezo 10 wakishika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.
Wamefunga mabao 26 ikionesha namna safu yao ya ushambuliaji sio mbaya sana inaweza kufunga lakini pia, kwenye ulinzi wamekuwa wakiruhusu mabao sana wakifungwa mabao 38. Mtibwa iliifunga KMC bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro na kukata tiketi ya robo fainali. Timu hizi katika mara saba zilizokutana, Azam imeshinda mara saba na Mtibwa mara tatu zikitoka sare nne.
Wenyeji Azam FC wamewahi kutwaa taji la FA mara moja mwaka 2018/2019 na leo wanaweza kupewa nafasi kwa sababu ya faida ya kuwa katika uwanja wa nyumbani lakini pia, kiufundi wako vizuri ukilinganisha na wapinzani wao. Ingawa wakati mwingine aliyebora anaweza kuonekana mbovu siku hiyo kutegemea na alivyojiandaa kimbinu dhidi ya mwenzake. Hata Mtibwa hawawezi kubweteka wanajua wanacheza na timu ya aina gani hivyo watajipanga vizuri na pengine wakashinda kwa mpinzani. Mtibwa wana historia katika kombe hili kwani waliwahi kulitwaa mwaka 2017/2018 hivyo huenda wakapambana kwa vyovyote vile kufika nusu fainali na pengine fainali.
Mshindi wa mchezo huu atakutana na mshindi wamchezo kati ya Simba na Ihefu utakaochezwa wiki ijayo