WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ameipongeza Benki ya Mwanga Hakika (MHB) kwa kuendelea kutanua mtandao wake ambao hadi sasa umeigusa sekta ya miundombuinu na wajasiriamali wadogo wadogo.
Dk Mwigulu aliyasema hayo jijini Arusha Jumapili wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo kuongeza kuwa kuendelea kuongeza mtandao huo kunatoa fursa ya kuwafikia watu mbalimbali.
“Napenda kuipongeza benki ya Mwanga Hakika kwa jitihada zake za kujitanua na hivyo kutoa fursa za wananchi wa kada mbali mbali kufikiwa na huduma za kifedha pamoja na kusaidia swekta mbali mbali ikiwamo ujenzi wa miundo mbinu,” alisema Dr Mwiguli ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo lililofanyika katikati ya jiji la Arusha.
Kuzinduliwa kwa tawi hilo kunaifanya taasisi hiyo ya kifedha kuwa na jumla ya matawi saba.
Mbali na Arusha, matawi mengine yapo Dar es Salaam, Moshi, Dodoma, Mwanga na Same.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Jagjit Singh alisema tawi hilo litaweza kurahisisha huduma kwa wateja wake na wakazi wa Arusha kwa ujumla.
“Tawi hili la hapa Arusha litarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa kuwa lipo kati kati ya jiji. Tawi ni la kisasa na lina sehemu maalum kwa ajili ya wateja wakubwa, vifaa vya kisasa, huduma ya kubadilisha fedha nakadhalika. Hii yote ni kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata huduma bora za kisasa na kwa urahisi,” alisema.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa tawi hilo limefunguliwa mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa fursa za kiuchumi zilizopo jijini Arusha zinaweza kuwafaidisha wakazi wa jiji hilo.
“Tawi linalozinduliwa leo ni sehemu ya mkakati wetu wa kujitanua na kuwafikia wateja wengi zaidi. Lengo letu ni kuwafikia wateja popote pale walipo lakini pia tukizingatia utoaji wa huduma bora za kifedha zinazoendana na mahitaji yao,” alifafanua.