TAASISI ya Jiolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST) imetoa toleo jipya la kitabu kinachoonesha madini yanayopatikana nchini Tanzania kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata hadi Kijiji.
Akizungumza katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ‘sabasaba, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amesema toleo hilo la tano limetoka mwaka huu wa 2023 likiwa limebeba taarifa nyingi zinazoonesha madini yanayopatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Dkt. Budeba amesema tofauti na toleo ya nne, toleo jipya ambalo ni la tano limesheheni taarifa nyingi zaidi na lina ramani ya kila Mkoa inayoonesha jiolojia na madini yapatikanayo katika mikoa husika.
Amesema, kitabu hicho kinaonesha aina zote za madini yakiwemo ya ujenzi , viwandani, vito na madini mkakati.
Dkt.Budeba alifafanua kuwa toleo husika linategemewa kuendelea kuongeza uelewa wa wananchi na wadau wengine juu ya jiolojia na madini yanayopatikana katika maeneo yao na hivyo kuchochea uwekezaji katika sekta ya madini.
“Kupitia msimu huu wa sabasaba, GST imeendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa wachimbaji wa madini juu ya umuhimu wa kutumia taarifa zinazotokana na tafiti za madini zinazofanywa na GST ili kuongeza tija katika shughuli zao.”Amesema
Sambamba na utafiti wa madini , GST pia ina maabara ya kisasa inayotoa huduma za uchunguzi wa sampuli za miamba, madini, udongo na maji. Aidha, GST inajukumu la kuratibu majanga ya asili ya jiolojia kama matetemeko ya ardhi, milipuko ya volkano na maporomoko ya udongo na kutoa ushauri wa kitaalam juu namna bora ya kupunguza athari zake.
Comments are closed.