BMH yaweka mlango bandia wa moyo

DODOMA: Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanya upasuaji wa kuweka mlango wa bandia kwenye moyo na kuwa hospitali ya pili nchini kuanzisha huduma hiyo.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo BMH, Ahmed Toure, akizungumza leo Februari 16, 2024 amesema upasuaji huo umefanyika baada ya milango ya kwenye moyo inakuwa imeziba.

“Hivyo tumetoa mlango ulioziba ambao kitaalamu unaitwa valve na kuweka mlango wa bandia ili kuruhusu damu kuendelea kupita,” amesema Dk Toure.

Advertisement

Amesema, upasuaji huo umefanyika kwenye kambi ya pamoja ya matibabu ya moyo kati ya madaktari wa BMH kwa kushirikiana na wenzao kutoka Uholonzi.

Dk Toure amesema kuwa mlango huo unapobadilishwa mgonjwa anapona tatizo lililokuwa linamsumbua la mlango kuziba na damu itapita vizuri kama zamani.

“Mlango huu wa bandia ataishi nao maisha yake yote, na mzunguko wa damu unarudi kuwa wa kawaida,” anasema.

Kambi hiyo ya moyo ya wiki moja iliyoanza Jumatatu inatarajiwa kukamilika leo Ijumaa.