Mitambo ya kuchimbia gesi yanukia Bandari Mtwara

MTWARA. Kwa mara ya kwanza katika historia, Bandari ya Mtwara inatarajiwa kuanza kupokea mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa gesi asilia katika eneo la Nanguruwe, Mkoa wa Mtwara.

Hatua hiyo imebainika baada ya ugeni wa wafanyabiashara na viongozi wa Kampuni ya ARA Petroleum Tanzania kufanya ziara maalumu katika Bandari ya Mtwara kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa za mitambo ya mradi huo kuanzia Agosti, 2026.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Meneja wa ARA Petroleum Tanzania, Hilal Al Hinai, amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kutathmini miundombinu, vitendea kazi pamoja na ufanisi wa bandari katika kushughulikia mizigo mizito na mikubwa.

“Tumefanya ziara katika Bandari ya Mtwara ili kujiridhisha na uwezo wake wa kuhudumia shehena kubwa za mitambo ya uchimbaji wa gesi. Tumeridhishwa na miundombinu na maandalizi yaliyopo,” amesema Hilal.

Amefafanua kuwa kuanzia mwezi Agosti, 2026, kampuni hiyo inatarajia kuanza kupokea meli zitakazobeba vifaa vya mradi huo, ambapo kila meli itakuwa na zaidi ya tani 1,000 za mitambo na vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika uchimbaji wa gesi eneo la Nanguruwe.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Idara ya Masoko, Faraji Mbulalina, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari hiyo, akieleza kuwa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena mbalimbali kwa ufanisi.

Amesema Bandari ya Mtwara imeendelea kuboreshwa na kwa sasa ina unafuu wa tozo za kibandari, miundombinu wezeshi, vitendea kazi vya kisasa pamoja na rasilimali watu wenye ujuzi na weledi wa hali ya juu, hivyo kuwa chaguo sahihi kwa miradi mikubwa ya kimkakati.

ARA Petroleum Tanzania ni kampuni ya uchimbaji na uzalishaji wa mafuta na gesi, inayojihusisha na maendeleo ya rasilimali za gesi asilia katika eneo la Ntorya – Mtwara Kusini.

Kampuni hiyo ni tawi la ARA Petroleum yenye makao yake nchini Oman, iliyoanzishwa kusimamia na kuendeleza mradi wa gesi uliogunduliwa chini ya Ruvuma Production Sharing Agreement (PSA).

Mradi wa gesi wa Ntorya, ukikamilika, unatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa gesi nchini Tanzania, kuchangia uzalishaji wa umeme, kukuza sekta ya viwanda pamoja na kuimarisha usalama wa nishati na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kwa kifupi, ujio wa mitambo ya uchimbaji wa gesi kupitia Bandari ya Mtwara ni hatua muhimu katika maandalizi ya uzalishaji wa gesi asilia, unaoashiria fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi kwa Mkoa wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button